TZS 464 bilioni zatengwa kwa wanufaika 145,000
NA ISMAIL NGAYONGA – HESLB
BODI ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) imetangaza kuanza kupokea maombi ya mikopo kwa njia ya mtandao kwa mwaka wa masomo 2020/2021 kuanzia juzi hadi Agosti 31, 2020.
Akizungumza na wanahabari katika ofisi za HESLB zilizopo eneo la TAZARA jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB Abdul-Razaq Badru amesema waombaji wote wa mkopo wanashauriwa kusoma na kuuzingatia ‘Mwongozo wa Utoaji Mikopo kwa 2020-2021’ unaopatikana katika tovuti ya HESLB (www.heslb.go.tz).
“Mwombaji anaweza kuingia kwenye mfumo wetu kupitia tovuti yetu ambayo ni www.heslb.go.tz na atapata maelekezo ya kutosha ya kuingia katika mfumo wa OLAS – Online Loan Application System,” amesema Badru.
Kuhusu bajeti ya fedha za mikopo, Badru amesema Serikali imetenga TZS 464 bilioni kwa mwaka 2020/2021 ambazo zinatarajia kuwanufaisha jumla ya wanafunzi 145,000. Kati yao 54,000, watakua ni mwaka wa kwanza na wengine 91,000 ni wanaoendelea na masomo.
“Bajeti hii ya TZS 464 bilioni kwa 2020/2021 imeongezeka kutoka TZS 450 bilioni mwaka 2019/2020 ambazo zinawanufaisha jumla ya wanafunzi 132,119,” amesema Badru wakati akifafanua swali la mwanahabari aliyetaka kujua iwapo kuna ongezeko la bajeti.