Wasema ana dhamira kuzidisha kasi ya maendeleo

NA MWANTANGA AME

HOTUBA ya mgombea urais wa Zanzibar kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM), Dk. Hussein Mwinyi, imewapa matumaini wananchi wa Zanzibar hasa baada ya kuazimia kufanya mabadiliko yatakayoiletea maendeleo nchi.

Wakizungumza na Zanzibar Leo, ikiwa ni siku moja tu baada ya mgombea huyo kutambulishwa rasmi hapa Zanzibar, baadhi ya wananchi walisema hatuba yake imejaa matumaini makubwa kwa maendeleo ya Zanzibar.

Mmoja ya wananchi hao, Dk. Suleiman Haji Suleiman, alisema mambo matatu makubwa ambayo aliyaainisha yameonyesha kuwa Dk. Mwinyi ana dhamira ya dhati ya kuwatumikia wananchi wa Zanzibar hasa katika kupiga vita rushwa.

Aidha alisema hotuba yake imeonesha dira ya maendeleo kwa kukubali kuyalinda mapinduzi ya Zanzibar ambayo yanapinga vitendo vya rushwa na ubaguzi.

Alisema anachozingatia zaidi katika uwajibikaji wake ni kusimamia sera za serikali zilizowekwa na kinachohitajika kwa wananchi wa Zanzibar kutumia akili zao kuyakubali mabadiliko yatakayotokea.

Alisema siasa za Zanzibar zinaeleweka kwani katika chaguzi zilizowahi kufanyika CCM na CUF vlikuwa vinapishana kidogo katika kumpata mshindi, jambo ambalo lilisababisha serikali kuamua kuunda serikali ya umoja wa kitaifa.

Alisema lengo la serikali kuukubali mfumo huo ulikuwa ni kudumisha amani ya nchi na kuwapa nafasi wananchi wa Zanzibar kufanya shughuli zao za maendeleo huku huduma za kijamii zikiwemo za afya, maji zikipatikana kwa wakati na sio vurugu zilizokuwa zikitokea.

Alisema kitendo alichokifanya Dk. Mwinyi kuwakumbatia washindani wake alioingia nao katika kinyang’anyiro cha kuwania nafasi hiyo, bado hakitoi nafasi kwa chama chake kuendelea kumkataa kwani jambo hilo ni zuri kwa maendeleo na uhai wa chama chake kwani walimuahidi kushirikiana nae.

Alisema utaratibu wa hivi sasa kujitokeza kwa wingi kuwania nafasi za uongozi ni kutokana na kuwepo uwazi utakaowafanya wanachama wake kushiriki kwa wingi huku wakijua kwamba wanaotakiwa ni viongozi bora watakaoweza kuwatumikia wananchi hapo baadae.