NAIROBI, KENYA
SHIRIKA la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani (WFP), limesema idadi ya wakenya wasio na uhakika wa chakula na kuhitaji msaada wa haraka wa kibinadamu umeongezeka zaidi ya mara mbili mwaka huu.
Taarifa iliyotolewa na Mpango wa Chakula Duniani (WFP) mjini Geneva Uswisi ilieleza kuwa,, mwishoni mwa mwaka 2019 kulikuwa na Wakenya milioni 1.3 walioathirika vibaya na ukosefu wa chakula, lakini sasa shirika hilo linasema kuwa, mwezi huu wa Julai idadi inatarajiwa kuongezeka na kufikia kati ya milioni tatu hadi milioni 3.5 wakati familia zitakapoishiwa kabisa chakula msimu wa ukata utakapofikia kilele.
Kwa kusaidia juhudi za Serikali ya Kenya ambayo kwa sasa inapambana na janga la corona WFP ,inatoa msaada wa fedha taslimu za miezi mitatu kwa watu 279,000 wanaoishi katika makaazi yasiyo rasmi mjini Nairobi kwa familia ambazo tayari zilikuwa zinahaha kujilisha hata kabla ya janga la corona.
Kwa kushirikiana na shirika la kuhudumia watoto la Umoja wa Mataifa UNICEF na Wizara ya afya ya Kenya,WFP pia itatoa msaada wa chakula cha kutibu watoto wa chini ya miaka mitano 16,000 walio na utapiamlo uliopindukia, kina mama wajawazito na wanaonyonyesha 5,700 na wazee 6,800 ambao wanaishi kwenye makaazi duni.
Ili kufanikisha hilo WFP inahitaji dola milioni 33.9 kuhakikisha chakula na lishe sio tu raia wa Nairobi kwenye makaazi yasiyo rasmi bali kupanua wigo wa msaada kwa maeneo mengine kama Mombasa, Nakuru, Kilifi na Kwale.