NA LAYLAT KHALFAN

BARAZA la Manispaa Mjini, limewataka walimu wa skuli za maandalizi na msingi kuchukua tahadhari na utaratibu uliokua bora kwa wanafunzi juu ya usafi wa skuli.

Mkurugenzi wa Baraza hilo, Said Juma Ahmada, aliyasema hayo wakati alipokuwa akizungumza na walimu wakuu wa skuli hizo katika ukumbi wa Baraza la Manispaa Malindi Mjini Zanzibar.

Alisema suala la usafi maskulini linahitaji uangalifu wa hali ya juu hususan kwa watoto wadogo kwa kuwa bado wao hawajaweza kuchanganua sehemu safi na chafu.

Aidha, aliwataka walimu kuhakikisha wanatoa taarifa mapema kwa baraza hilo kama kutakuwa na upungufu wa vifaa vya kufanyia usafi ili kuimarisha mazingira katika maeneo mbalimbali yaliyozunguka skuli hizo.

“Mhakikishe skuli zinakuwa safi vyoo pamoja na madarasa na kama kutakuwa na upungufu wa vifaa msisiste kufika hapa, kwani bila usafi hakutakuwa na mzingira salama ya kufundishia”, alisema Mkurugenzi.

Naye Msaidizi Mkurugenzi wa Elimu wa baraza hilo, Kibibi Mohamed Mbarouk , alisema kwa mwaka huu skuli zitakuwa wazi kusomesha hadi Disemba kwa vile skuli zilifungwa kipindi kirefu kufuatia kuwepo kwa maradhi ya maambukizi ya virusi vya Corona.

Sambamba na hayo aliwataka walimu kuongeza bidii ya ufundishaji  ndani ya skuli hizo, kwani wanafunzi walichukua muda mwingi kukaa majumbani.

“Walimu jukumu lenu ni kuwasimamia wanafunzi na msichoke kwani tunahitaji vijana bora watakaoweza kulijenga  taifa bora la kesho’, alisema.