MWAKA 2020 ukitafahamika kama mwaka wa uchaguzi hapa nchini utakaowaingiza maradakani viongozi wa kisiasa kwa muda wa miaka mitano ijayo, hatua tuliyo nayo hivi sasa ni vyama vya siasa viko kwenye hatua mbalimbali za kupata wagombe.

Vipo vyama vya siasa vimeshamaliza mchakato wa kuwapata wagombea urais, ambapo vyama hivyo vinasubiri ruhusa ya Tume za Uchaguzi tayari kwa ajili ya kampeni.

Lakini kwa ujumla kazi inayoendelea hivi sasa katika vyama vya siasa kutafuta wagombea ambao watawakilisha vyama vyao kwenye nafasi za ubunge, uwakilishi na udiwani.

Kwenye ofisi za vyama makada wa vyama wanamiminika kuchukua fomu za kutaka ridhaa ya kuwawakilisha wananchi katika vyombo vya kutunga sheria na kwenye mabaraza ya mji.

Hata hivyo tungependa sana kuvieleza vyama vya siasa na wachama wa vyama hivyo wahakikishe wanawachagua watu ambao kweli wana sifa na uwezo wa kuwatumikia watu.

Vyama katika kipitisha wagombea na wanachama katika kura za maoni za kuwapima wagombea, lazima wazingatie sifa za mbunge, mwakilishi na diwani wanayempitisha na wajiridhishe je wana uwezo wa kazi wanayoiomba?

Utumishi wa kisiasa ukiwemo ubunge na uwakilishi, umekuwa na maslahi makubwa sana ya kifedha, hivyo kutokana sababu hiyo kila mmoja amekuwa akivutiwa kupata maslahi hayo na kupitikiwa kabisa na suala la kuwatumikia watu.

Kwa maana hiyo wengi wenye nia na waliokwisha chukua fomu za kuwania nafasi hizo lengo lao ni kupata maslahi inayoambatana na mishahara na maposho makubwa ya vikao vya mara kwa mara.

Ili tuweze kuepukana na viongozi wanaojali matumbo yao na wabinafsi, wakati ndio huu kwa wanaowapima wagombea wahakikishe viongozi wa namna hiyo wanawaacha kwa sababu hawana faida kwa vyama vyenyewe na wananchi kwa ujumla.

Kwa upande mwengine ili tuwe na serikali imara kwa upande wa Jamhuri na serikali ya Mapinduzi, vyama pia vingezingatia kuwapa nafasi watu wenye taaluma waliokwenda skuli vizuri wakiwemo wanawake.

Hatupingi suala la sifa za msingi za kuwa mbunge ua mwakilishi ni kujua kusoma na kuandika, lakini kwa kasi ya dunia na nchi yetu inakotaka kwenda lazima tujiulize kweli sifa hizi tunapaswa tuendelee nazo kwa wakati huu?

Huwa haipendezi kwa marais wetu wakati wanatafuta watu wa kutengeneza baraza la mawaziri kwa serikali zetu, wanajikuta kwenye wakati mgumu watu waliochaguliwa hawana sifa timilifu za kuwa mawaziri.

Wakati mwengine inakuwa aibu pale waziri anaposhindwa kujieleza kwenye mikutano mikubwa ya kimataifa ya kuiwakilisha nchi kwa sababu ya uelewa na upeo mdogo wa mambo unaotokana na sifa zilizompa ubunge au uwakilishi za kujua kusoma na kuandika.

Ukiachilia mbali wapo wabunge na wawakilishi kwa hakika kabisa walishindwa hata kuzungumza, kuchangia na kujenga hoja ukichunguza utabaini moja ya sababu ni sifa walizonaso za kujua kusoma na kuandika.

Tunalazimika kueleza haya kwa sababu ukweli ni kwamba za kujua kusoma na kuandika kwa mbunge ama mwakilishi ni nyepesi sana na umefika wakati wa mabadiliko.