NEW DELHI,INDIA

INDIA na Umoja wa Ulaya zimekubaliana kuanzisha mazungumzo ya ngazi ya juu ya mawaziri kuhusu biashara na uwekezaji.

Pande hizo mbili ziliafikiana hatua hiyo wakati wa mkutano wa kilele uliofanyika kwa njia ya video.

Hata hivyo washiriki wa mkutano huo hawakutoa tarehe kamili ya kuanzisha mazungumzo hayo ya biashara huru ambayo yalikwama kwa muda mrefu.

Mkutano kwa njia ya video uliongozwa na Waziri Mkuu wa India Narendra Modi, rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Ulaya Charles Michel, pamoja na rais wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya Ursula von der Leyen.

Taarifa ya pamoja iliyotolewa baada ya mkutano huo ilisema mazungumzo hayo ya ngazi ya juu yatalenga kukuza makubaliano kuhusu biashara na uwekezaji, kuondoa visiki vya biashara na kuimarisha mazingira kwa wafanyabiashara na wawekezaji kutoka pande zote mbili.