TEHRAN,IRAN

WATAFITI na wataalamu wa Iran wamevumbua kifaa kipya cha kugundua haraka waathiriwa wa corona bila ya kuwa na alama na viashiria vyovyote vya ugonjwa huo.

Shirika la habari la ISNA limeripoti habari hiyo na kuongeza kuwa, kifaa hicho kinafanyia uchunguzi kiwango cha aina za oksijeni iliyopo katika koo la mtu na kujua mtu huyo ni muathiriwa wa COVID-19 au la.

Kuongezeka aina ya oksijeni katika koo la mtu ni moja ya vielelezo vya uwezekano wa kuathiriwa na corona kwani wagonjwa wa COVID-19 hata kama hawajaanza kuonesha alama zozote za ugonjwa huo, kiwango cha oksijeni kwenye koo la mgonjwa hubadilika na kwamba sensa inayozalishwa na kielelezo hicho inaweza kuonesha iwapo mtu ni mgonjwa wa corona au la.

Kifaa hicho kipya kilifanyiwa majaribio kwa wagonjwa 600 katika hospitali nne nchini Iran na kimetoa majibu mazuri na ya kuridhisha.

Kifaa hicho hakigundui wagonjwa wa COVID-19 tu, bali kinagundua pia wagonjwa wa maradhi ya mapafu na mengineyo.

Takwimu zinaonesha kuwa, hadi hivi sasa wagonjwa 257,303 wa COVID-19 waligunduliwa nchini Iran kati ya hao, wagonjwa 219,993 washapata nafuu na kuruhusiwa kurudi nyumbani.

Marekani ndiyo inayoongoza kwa mbali kwa idadi kubwa ya wagonjwa na vifo vya corona duniani ikifuatiwa na Brazil. Nchi za Ulaya za Uingereza, Italia na Ufaransa zinafuatia kwa idadi kubwa zaidi ya vifo vya corona duniani.