UJENZI wa uwanja wa michezo wa Mao Zedong uliojengwa kwa ufadhili wa Serikali ya China na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, tayari umekamilika na hivi sasa uendelea kutumika na kutoa faraja kwa wanamichezo mbalimbali nchini.
Kukamilika kwa uwanja huo, kuliongeza idadi ya viwanja vya kisasa kufikia vitatu ukiwemo uwanja wa Amaan na Gombani, Pemba.
Tungelipenda kuwapongeza ndugu zetu wa China kwa namna walivyokubali kuujenga tena uwanja huo ambao awali ulikuwepo huko nyuma kama uwanja pekee uliokuwa ukitumika hata kwenye michuano ya Kombe la Goseji kwa wakati huo kabla ya kuchakaa na kupotea kabisa.
Lakini kwa ujenzi wa sasa, uwanja huo umejumuisha michezo mengine midogo midogo ya ndani na hivyo kutoa fursa zaidi ya kuendeleza michezo nchini.
Bila ya shaka uwanja huo umepunguza tatizo la kuwepo kwa viwanja vya kisasa vya michezo hasa ya ndani liliopo visiwani hapa.
Lakini pamoja na hali hiyo njema, kumejitokeza tatizo kidogo la kuwepo kwa jaa pembeni mwa uwanja huo na hivyo kwa kiasi kikubwa kupoteza haiba ya uwanja huo ambao ni matarajio ya wengi kwamba utakuwa kichocheo cha kukuza na kuimarisha michezo.
Zanzibar Leo kama jamii ya wanamichezo haturidhishwi na mandhari ya uwanja huo kutokana na kuwepo kwa jaa hilo ambalo pia linachangia kuharibu mazingira kutokana na aina ya taka zinazotupwa zikiwemo ‘pempasi’ za vinyesi nk.
Kama utatembelea uwanja huo hivi sasa utaona jinsi gani Mao unavyopendeza kwa rangi na muonekano wake, lakini, sifa hizo sasa hazina maana kutokana na vitendo vya kutupa taka kwenye eneo hilo.
Kwa maneno mafupi na yalionyooka, kitendo cha kutupa taka katika uwanja huo kwa kweli hakikubaliki na hakileti picha nzuri na tuweke wazi kuwa kinatia doa kwa uwanja huo.
Sasa tunaamini kujitokeza hilo, mamlaka zinazohusika zitalifanyia kazi na kutafuta mahali pengine pa kulihamishia jaa hilo ili kurejesha haiba ya uwanja huo.
Lazima tufikie mahali na kujikubalisha kwamba mjenga nchi ni mwananchi mwenyewe na sote tuwajibike katika kuliona hili kwa ajili ya maendeleo ya taifa na wananchi wake.
Tuna imani kubwa kwamba, uwanja huu utatuanzia ukurasa mpya wa kuibua vipaji vipya ambavyo vinaweza kuwika tena katika michezo Zanzibar huku vipaji viliopo vikihitaji kuendelezwa ili viweze kuonekana.
Zanzibar yenye mafanikio ya michezo inawezekana ikiwa kila mmoja wetu atatimiza wajibu wake.