NA HANIFA SALIM

WATU wenye majitaji maalumu nchini wana kila sababu ya kushirikishwa na kupewa kipaumbele zaidi katika miradi ya maendeleo ili kupata mbinu za kujiinua kiuchumi.


Msaidizi Mkurugenzi masuala ya mtambuka katiba baraza la mji Chake Chake Tifli Mustafa Nahoda, aliyasema hayo wakati akikabidhi vifaa kwa vikundi vya watu wenye mahitaji maalumu katika ukumbi wa baraza hilo Chake Chake.


Alisema, ni vyema jamii kuvipa kipaumbele vikundi vya ujasiriamali vya watu wenye mahitaji maalumu, ili kuwashirikisha katika nyanja mbali mbali za maendeleo.

Alisema, idara ya mtambuka inashughulikia masuala ya kijamii ambayo yanajulikana kitaifa ikiwemo udhalilishaji, dawa za kulevya, mazingira, maradhi ya mripuko, maafa na watu wenye mahitaji maalumu.

“Yanapotolewa mafunzo kwa wajasiriamali na vikundi vya wajasiriamali wenye majitaji maalumu, lazima vishirikishweni kwa sababu na nyinyi ni wajasiriamali na mna haki kama nyengine,”alisema.

Aidha aliitaka jamii inapoona tatizo la udhalilishaji kwa watu wenye mahitaji maalumu kutoyafumbia macho kwani badala yake wayaripoti kwa taasisi husika.


Mwalimu Mkubwa Ahmed Omar kutoka kikundi cha ufugaji kuku wa kienyeji Vitongoji, aliipongeza idara ya mtambuka kwa kuvijali vikundi vya watu wenye mahitaji maalumu kwa kuwapatia mafunzo, kuwatembelea na
kuwapatia vifaa ambavyo vitatumika katika uzalishaji.

“Tunashukuru sana, tunaendelea kufuata maelekezo kutoka kwenu ili tuweze kwenda vizuri zaidi na tunaomba msiishie hapa muendelee kutuunga mkono na wengine wajitokeze kwetu tutawapokea na tutafarajika zaidi,” alisema.