TEHRAN,IRAN

HUKUMU ya kumnyonga jasusi wa Shirika Kuu la Kijasusi la Marekani CIA, na Shirika la Kijasusi la Utawala wa Israel, Mossad, imetekelezwa jana asubuhi.

Kwa mujibu wa taarifa, Mahmoud Mousavi Majd ambaye alipatikana na hatia ya kushirikiana na mashirika ya kijasusi ya CIA na Mossad, alinyongwa jana asubuhi nchini Iran.

Kesi ya jasusi huyo ilikuwa inasikilizwa na Mahakama ya Mapinduzi ambayo iliamuru anyongwe.

Mousavi Majd alikamatwa Oktoba 10 mwaka 2018 na kesi yake ikaanza kusikilizwa katika Tawi la 15 la Mahakama ya Mapinduzi ya Kiislamu na hatimaye baada ya mahakama kumpata na hatia, hukumu yake ya kunyongwa ilitolewa Agosti 25 mwaka 2019.

Hukumu hiyo ya kunyongwa ilipitia michakato kadhaa ya kisheria katika Mahakama ya Kilele ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ambayo iliidhinisha utekelezwaji wake.