NA ZUHURA JUMA

JUMUIYA ya Maimamu wilaya ya Chake-Chake (JUMAZA) imewataka wazazi na walezi kisiwani Pemba kufanya mambo yao kwa kufuata taratibu na miongozo ya dini ya kiislamu katika kipindi cha sikukuu ya Eid-el-Hajj, ili kuwakinga watoto na udhalilishaji.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwao Chake Chake, Katibu wa Kamati ya Maadili kutoka JUMAZA, Sheikh Abdalla Mnubi Abas, alisema kamati haimzuii mtu kutembea lakini cha muhimu ni kuwalinda watoto dhidi ya udhalilishaji.

Alieleza kuwa, kipindi cha sikukuu watoto wengi hufanyiwa
udhalilishaji, hivyo ni vyema kwa wazazi na walezi kufuata taratibu na miongozo ya kiislamu ambayo itasaidia kuwalinda watoto wao na janga hilo.


“Inapomaliza sikukuu tunapata kesi nyingi za watoto wetu kufanyiwa udhalilishaji, hivyo tutakapofuata taratibu ya dini yetu ya kiislamu tutawadhibiti,” alisema.

Alisema katika kuwadhibiti watoto hao ni vyema wakaongozana nao katika viwanja vya kufurahishia watoto, jambo ambalo litasaidia kwa kiasi kikubwa kuepuka vishawishi.

“Watoto wanatoka peke yao bila usimamizi wa wazazi, hii ni hatari kubwa kwao, hivyo tukawatembeze watoto wetu,” alieleza.

Aidha aliitaka jamii isifanye mambo yalio nje ya utaratibu wa dini ya kiislamu na waende na mfumo ambao hautaathiri jamii.

Kwa upande wake, Naibu Amiri kutoka JUMAZA, Sheikh Seif Khamis Nassor aliiomba serikali kuwaruhusu watoto kutembea kuanzia saa 1:00 asubuhi hadi saa 12:30 jioni, ili kuwaepusha kufanyiwa vitendo vya udhalilishaji.

“Mara nyingi udhalilishaji hufanyika nyakati za usiku, hivyo viwanja vya kufurahishia watoto ni vyema tukavifungua asubuhi na kuvifunga magharibi,” alisema.