NA ASIA MWALIM

JUMUIYA ya Wastaafu Zanzibar (JUWAZA) imepongeza Dk. Hussein Ali Mwinyi kwa kuteuliwa kuwa mgombea Urais wa Zanzibar kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi.

Alisema imani yao kwa Dk. Hussein ni kuendeleza mambo mazuri, kuimarisha zaidi baadhi ya mambo yaliyokuwa hayajakamilika, yatakayo achwa na Rais wa Zanzibar Dk. Ali Mohammed Shein, kwa kutekeleza ilani ya chama hicho.

Katibu wa Jumiya hiyo, Salama Kombo Ahmed, aliyasema hayo alipokua akizungumza na muandishi wa habari hizi huko ofisini kwake Kilimani Mjini Zanzibar.

Alisema ikiwa Dk. Hussein atachaguliwa kuwa Rais wa Zanzibar ni vyema kuliangalia suala la wazee na mustakabali wao kwa kuwaongezea pencheni wastaafu, ili wapate kima cha chini cha mfanyakazi.

Katibu huyo alimuomba kuweka mfuko maalumu wa wazee kama waliowekewa vijana, ili kutatua changamoto zinazo wakabili kwa wakati huu, ikiwa pamoja na kufanya haraka kupatiwa vitambulisho maalum vya wazee ambavyo havijakamilika, ili iweze kuwa rahisi kutambuliwa wanapokua wanatafuta huduma zao.

“Wazee watakapo patiwa vitambulisho maalumu wataweza kupata huduma wanazozihitaji kwa uzuri, zikiwemo za usafiri kwenye magari ya umma pamoja na matibabu wanapokuwa Hospitali” alisema.

Sambamba na hayo amevitaka vyama vya siasa nchini kutanguliza suala la amani, kwa kuweka mshikamo kati ya washindani wanaogombania nafasi za uongozi mbalimbali, ili kuwepo mshikamano baina yao.

“Ili nchi iendelee kuwa na amani jambo muhimu kwa wananchi ni kushikaman, kueka urafiki kati ya ataeshinda na atakae shindwa kwenye kinyangnyiro hicho” alisema.

Hata hivyo, amewataka viongozi wa vyama vya siasa wanaotarajia kufanya kampeni zao nchini, kuacha ugomvi ili kuepusha kuwachanganya wananchi na kuwatia hofu.