KHARTOUM,SUDAN

MIILI ya maofisa wa jeshi 28 ambao wanatajwa kuhusika na jaribio la mapinduzi lililoshindwa dhidi ya rais wa zamani wa Sudan Omar al-Bashir mwaka 1990 imekutwa katika kaburi la pamoja.

Taarifa hiyo ni kwa mujibu wa mwendesha mashitaka wa umma.

Taarifa zinaeleza kuwa hilo ni kaburi la pili kugundulika, tangu Bashir, ambae aliliongoza taifa hilo kwa mkono wa chuma kwa miongo mitatu, aondolewe madarakani kutokana na shinikizo la maandamano ya umma.

Mwendesha mashitaka wa umma Tagelsir al-Hebr alisema ikiwa kama sehemu ya jitihada za uchunguzi za uovu uliofanywa na Bashir miili hiyo ilipatikana Omdurman, mji pacha na ule mji mkuu wa Khartoum.

Anasema zoezi la ugunduzi lilifanywa na wachunguzi 22 kutoka katika tasnia mbalimbali na lilichukua wiki tatu hadi kugundulika.

Inaelezwa Aprili 1990 maofisa wa jeshi walilizingira eneo la makao makuu ya jeshi na makambi kadhaa kabla hawajakamatwa na kuuwawa.