NA MWANAJUMA MMANGA

MKURUGENZI  Idara ya Misitu  Maliasili  Zisizoejesheka imeitaka Kamati  za hifadhi ya jamii  na  wanajamii  kushirikiana  pamoja  na Hamlmashauri Wilaya ya Kati Unguja, ili kuweza kuendeleza usimamizi na matumizi endelevu ya rasilimali hiyo.

Aliyasema hayo wakati akizungumza na Mwandishi wa Zanzibarleo huko Ofisini kwake Maruhubi Wilaya ya Magharib ‘A’ Unguja.

Alisema hatua hiyo itasaidia kubaki misitu hiyo kwani inaonekana kupotea kwa kiasi kikubwa rasilimali hiyo pamoja na  wanayama pori kupotea.

Alisema Changamoto kubwa iliyoonekana hivi sasa  katika hifadhi ya Kati na Kusini kumekuwa na  uvamizi wa msitu hiyo kwa shughuli za kilimo, pamoja na makaazi, lakini pia uvamizi wa ukataji ovyo wa misitu kwa ajili ya matumizi ya makaa na kuni hali ambayo inapelekekea kumalizika kwa kasi rasilimali hiyo.

Pia, alisema  kumejitokeza hali nyengine ya tamaa za watu kuvamia maeneo kwa ajili ya kujimilikisha, ili wauze kwa shughuli za uwekezaji hasa za kitalii, jambo ambalo liwarejeshe nyuma idara ya misitu.

Alisema iwapo misitu ya jamii itaimarika na kuhifadhika vizuri basi changamoto ya mabadiliko ya tabia nchi itasaidia kuondoka.

Alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, imefanya maamuzi hivi karibuni ya kuweza kugatua juu ya misitu ya hifadhi ya jamii kupelekwa katika halmashauri chini ya usimamizi wake  kwa Unguja na Pemba, ili kuona rasilimali hiyo inalindwa na inabaki kwa ajili ya sasa na vizazi vijavyo.