NAIROBI,KENYA

WIZARA  ya Afya nchini Kenya imesema itaongeza juhudi zaidi katika mpango wa kutoa huduma majumbani kama sehemu ya mkakati wa kupambana na virusi vya Corona, baada ya kushuhudia mafanikio yaliyopatikana kutokana na mpango huo.

Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Rashid Aman alisema mpango huo utatumika kupunguza msongamano katika vituo vya afya ambavyo vitatoa huduma kwa wagonjwa wenye maradhi mengine.

Alisema ingawa serikali inaendelea kuongeza hatua za kukabiliana na kuenea kwa virusi hivyo,mafanikio ya mpango huo kwa wale waliopata maambukizi yametoa mwanga mpya katika mapambano dhidi ya virusi hivyo.

Katibu Mkuu huyo alisema, jumla ya wagonjwa 2,738 waliopata matibabu wakiwa majumbani katika wiki moja iliyopita wamepona, na kuongeza kuwa kuna wagonjwa wengi zaidi waliowekwa kwenye mpango huo.

Hadi sasa, jumla ya kesi 14,805 za maambukizi ya virusi vya Corona zimethibitishwa nchini Kenya.