NAIROBI,KENYA

RAIS Uhuru Kenyatta wa Kenya amesema ataitisha kikao cha dharura kutathmini kuongezeka kwa maambukizi ya virusi vya Corona nchini humo.

Msemaji wa Ikulu ya Kenya  Kanze Dena alisema, kikao hicho cha tano cha uratibu kati ya serikali kuu na serikali za kaunti kitatathmini maandalizi ya kaunti ndani ya mfumo mpana wa kitaifa wa kukabiliana na janga hilo.

Alisema kikao hicho kiliitishwa kutokana kuongezeka kwa kasi ya maambukizi ya virusi vya Corona nchini humo, ambapo mpaka sasa kaunti 44 kati ya 47 nchini humo ziliripoti maambukizi hayo.

Alisema rais ,Kenyatta ametoa wito kwa Wakenya kuendelea kuvaa barakoa katika sehemu za umma, kutekeleza usafi wa mikono na uso kwa wakati wote, na kufuata miongozo na itifaki za kukaa mbali.

Hatua hiyo ilikuja wakati Wizara ya Afya nchini humo ikiripoti kesi mpya 418 za maambukizi ya virusi vya Corona, na kufanya idadi ya jumla ya maambukizi nchini Kenya kufikia 13,771.