NAIROBI, KENYA

WIZARA ya Afya ya Kenya imesema, jumla ya kesi zilizothibitishwa kuwa na virusi vya Corona nchini humo imefikia 15,601 baada ya watu 796 kukutwa na maambukizi, ikiwa ni idadi kubwa zaidi kurikodiwa kwa siku moja.

Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Mercy Mwangangi alisema,kesi hizo zinatokana na sampuli 6,754 zilizopimwa, na kufanya jumla ya sampuli zilizopimwa mpaka sasa kufikia 261,027.

Alisema kati ya kesi zilizokutwa na maambukizi 793 ni za raia wa Kenya na wengine watatu ni raia wa kigeni.

Wakati maambukizi ya virusi vya Corona yakiongezeka kwa kasi nchini Kenya, mamlaka za nchini humo ziliongeza hatua za udhibiti, ambazo baadhi ya wananchi walikuwa wakikiuka kuzifuata,ikiwemo kutovaa barakoa katika maeneo ya umma, na hivyo kuhatarisha maisha yao na ya wengine.

Mwangangi alisema, serikali itaanza kutembelea jamii mbalimbali na kutoa elimu kwa umma kuhusu kuzingatia hatua za udhibiti zilizowekwa na mamlaka husika.