NAIROBI,KENYA

WIZARA   ya Afya ya Kenya imesema imeanza kutumia app maalum ili kuwafuatilia watu walioambukizwa virusi vya Corona wakati vifo vilivyoripotiwa nchini humo kutokana na ugonjwa huo vimefikia 12, ikiwa ni idadi kubwa zaidi kwa siku.

Waziri wa Afya wa Kenya Mutahi Kagwe alisema wahudumu wa afya sasa wameacha kufuatilia watu kwa kuwapigia simu, na badala yake wanafuatilia kwa kutumia matumizi ya kompyuta na Internet.

Akiongea na waandishi wa habari mjini Nairobi, Kagwe alisema kikundi maalum cha taifa cha ufuatiliaji sasa kinapewa mafunzo ya kutumia mtandao wa internet na usimamizi wa data kwa ajili ya ufuatiliaji.

Alisema kwa sasa kuna vikundi 229 kwenye kaunti zote vinavyofanya kazi ya ufuatiliaji na uchunguzi.

Aliwataka wakenya watulie wakati idadi ya watu wanaoambukizwa inaongezeka, na kutopuuza mapambano dhidi ya virusi vya Corona.