BAMAKO,MALI

KESI  ya mpiganaji wa jihadi Mali anayeshitakiwa kwa kuharibu maeneo ya ibada mjini Timbuktu na kuanzisha  utawala wa ukandamizaji na mateso inaanza kusikilizwa katika Mahakama nya Kimataifa ya Uhalifu (ICC).

Al-Hassan ag Abdoul Aziz Mohamed Ag Mahmoud, mwenye umri wa miaka 42, alishitakiwa kwa  uhalifu wa kivita, uhalifu dhidi ya ubinadamu, ubakaji na utumwa wa kingono.

Mashitaka hayo yanaanzia wakati kundi la Waislamu wenye itikadi kali walipotumia mapambano ya  kundi la kabila la Tuareg mwaka 2012 kuikamata miji iliyoko katika hali tete upande wa kaskazini nchini  Mali.

Waendesha mashitaka katika mahakama mjini The Hague watatoa maelezo yao ya ufunguzi dhidi ya mtu waliyemwelezea katika kikao cha kabla kuwa aliwatesa sana wakaazi wa eneo hilo.