LIGI Kuu ya Zanzibar imerejea tena baada ya kusimamishwa kwa karibu miezi mitatu kutokana na janga la maradhi ya ‘corona’ yaliyoikumba dunia.

Michuano hiyo na mengine nchini ilisimama Machi 17, mwaka huu kutokana na kuwepo kwa janga hilo la ‘corona’ ambalo kwa kiasi kikubwa liliathiri shughuli za kiuchumi sambamba na michezo.

Ligi mbalimbali duniani zilisimama na nyengine kuahirishwa kabla ya kufutwa kabisa, lakini, sasa sasa hali kidogo imetoa ahueni na michezo kurejea kwa baadhi ya nchi.

Kurejea kwa michezo inamaanisha kwamba ugonjwa wa ‘corona’ kasi yake imepungua, lakini, haijaisha kabisa, hivyo, tahadhari bado zinatakiwa kuchukuliwa tena kwa kiwango cha juu.

Ni wazi kwamba kila nchi inapambana kwa namna yake, lakini, kupungua kwa maambukizi ni ishara kwamba nchi yetu imechukua hatua stahiki zaidi katika kukabiliana na janga hili.

Hivyo tunachukuwa nafasi hii kuzikumbusha klabu kuendelea kufuata maelekezo yanayotolewa na Wizara ya Afya katika kujikinga na maradhi hayo, ikiwemo kunawa mikono kwa wachezaji na kuepuka kukumbatiana ndani na nje ya uwanja.

Tunachoendelea kusisitizwa ni kwamba pamoja na kwamba ‘corona’ imepungua, lakini, bado ipo, hivyo ni vyema tukaendelea na tahadhari zote zinazoelekezwa na Wizara ya Afya juu ya maradhi hayo.

Itakuwa ni jambo la hatari kujisahau katikati ya vita huku mpira ukirejea na kuleta hamasa mpya kwa mashabiki na wadau wa mchezo huo.

Kutokana na hali hiyo, tunatakiwa kuzingatia na kuwa na tahadhari kubwa ili tuendelee kuona mpira na shughuli nyengine za ujenzi wa taifa.

Kurejea kwa mpira na shughuli nyengine za kijamii hakutoi tafsiri kwamba ‘corona’ haipo na kwamba watu wanaweza kwenda viwanjani bila ya kuchukua tahadhari.

Tunaelewa kwamba serikali bado haijaruhusu mashabiki kwenda viwanjani, lakini, kuzingatia kujitenga, yaani kukaa umbali wa mita moja kati ya mtu na mtu, litakuwa jambo bora zaidi.

Hivyo kwa wale watakaokuwa wakipata nafasi ya kwenda viwanjani, hawatakiwi kujisahau na kuanza kukaribiana, badala yake wachukue tahadhari kubwa kweli kweli kadri ya inavyowezekana.

Wahusika wote, wanatakiwa wawe makini kuhakikisha soka linachezwa kwa usalama na kwa kuzingatia kanuni zote za kiafya katika kipindi hiki cha ‘corona’.

Ile tabia ya mashabiki kukumbatiana baada ya goli kufungwa na kugongesheana mikono, katika kipindi hicho tunalazimika kuiacha ili mpira wetu uwe salama kama ambavyo serikali imepanga.

Tunafahamu mchezo wa soka unahusisha hamasa kubwa kutoka kwa mashabiki, lakini, isiwe kisingizio cha kutojali afya wakati huu mgumu tulionao tukielekea kushinda janga la ‘corona’.

Kila la heri Ligi Kuu ya Zanzibar, lakini, tusisahau corona bado ipo.