Mashindano machungu kwa timu za Zanzibar

NA ABOUD MAHMOUD

KOMBE la Mapinduzi moja ya mashindano maarufu nchini Tanzania ambayo yameonekana kuvutia mashabiki wengi, katika mchezo wa soka ukitoa ligi kuu ya Tanzania Bara na visiwani.

Mashindano hayo ya Mapinduzi ambapo hufanyika kila mwaka mwezi Januari huzikutanisha timu mbali mbali kutoka Tanzania Bara na Zanzibar.

Lengo la kuanzishwa mashindano hayo ni kuyaenzi Mapinduzi matukufu ya mwaka 1964, ambayo yaliweza kuondosha utawala wa kisultani na kuwapatia maendeleo wananchi wake.

Kwa miaka kadhaa hivi sasa mashindano hayo huandaliwa na hufanyika, ambapo mashabiki wa mchezo wa soka kutoka sehemu mbali mbali nchini Tanzania kuangalia timu zao zinaposhiriki kwa kuchukua ubingwa.

Zanzibar ndio waandaaji wa mashindano hayo ambapo timu mbali kutoka visiwani humu hushiriki, na katika kumbukumbu mwaka mmoja timu ya soka ya Miembeni ndio iliwahi kuchukua ubingwa huo.

Baada ya kuchukua ubingwa huo miaka yote kombe hilo huchukuliwa na timu mbali mbali kutoka Tanzania Bara, ikiwemo Simba,Yanga, Azam FC, Mtibwa Sugar na nyenginezo.

Lengo la kuandika makala haya ni kuonesha namna gani wadau wa soka wanavyolizungumzia kitendo cha timu za Zanzibar, kushindwa kuchukua kombe hilo kwa miaka mingi.

Suala hilo limeonekana kuwaathiri mashabiki hao kwani  wenyeji wa mashindano hutolewa mwanzo.

Kila mmoja amekuwa na mawazo yake ambayo yalionekana kumuumiza ndani ya moyo kwa kuona timu za nyumbani hazifanyi vyema kwenye mashindano hasa kwa kuwa wao ndio waanzilishi .

Katika Makala hii viongozi wa klabu,wachezaji wa zamani pamoja na wadau walitoa maoni yao juu ya suala hili, lakini walitoa maoni yao nini kifanyike ili kuweka utaratibu mzuri.

Salum Baussi mchezaji wa soka wa zamani na pia ni kocha mchezo huo alisema ni jambo la aibu sana kuona timu za Zanzibar zinaingia katika mashindano makubwa kama hayo lakini hazifiki popote.

Alisema kwamba tatizo kubwa linalofanya timu za Zanzibar kutofanya vizuri na kutolewa mapema ni kutojifahamu kwa kile  wanachokifanya na kuyaona mashindano hayo kama ligi za kawaida.

“Kwa kweli sio jambo zuri kwani miaka mingi tunaingia katika mashindano na sisi ndio wenye kombe, lakini tunatolewa mapema, tangu lilipochukuliwa na Miembeni mara moja halijachukuliwa na timu yoyote ya Unguja,”alisema.

Bausi alisema lazima wachezaji waache dharau kwani mazoezi,mechi za ligi kuu tofauti na kombe la Mapinduzi, kufanya dharau hakutoweza kusaidia kupanda timu za nyumbani.

Abdullah Juma Aley (Abdulwakati) alisema kwamba timu za Zanzibar zimekuwa zikilidharau kombe la Mapinduzi kwa kuona kama ni mechi za kirafiki na kushindwa kufika mbali.

Alisema wachezaji wengi wa Zanzibar hawajitumi na hawakubali kusikiliza makocha wao, ambao ndio msingi mkubwa wa kukuza vipaji vya wachezaji na kufikia malengo.

“Aibu tena aibu kubwa sana serikali inagharamika kuandaa mashindano hayo, inahangaika huku na kule kutafuta wadhamini halafu timu zetu zinafika hatua za mwanzo zinatolewa inaniuma sana,”

Abdulwakati alisema lazima makocha wa soka kwa kushirikiana na shirikisho la soka Zanzibar (ZFF), kuhakikisha timu zinajituma inavyotakiwa ili kuweza kufanya vizuri katika mashindano hayo.

Nae Mohammed Badru Mzanzibar anaefundisha soka nchini Uingereza alisema kombe la Mapinduzi ni la Watanzania wote, hivyo kuchukuliwa Tanzania Bara na kubakia nyumbani ni jambo la kawaida.

Badru alisema sio vibaya  kuchukuliwa Bara lakini dalili kubwa inaonesha kwamba wachezaji wa timu za Zanzibar,  hawajitumi katika mashindano kama hayo na kuyachukulia sawa na mechi za kirafiki.

“Lazima tuwe tunafahamu kwamba michezo tunayocheza hii ligi kuu au mechi za kirafiki,mashindano ya kimataifa na mashindano mengine hapo ndio tutajielewa, wenzetu Tanzania Bara wanajua nini wanachokifanya wanajituma lakini sisi nyumbani tunadharau ndo maana soka letu kila kukicha linashuka hadhi  kwa hiyo tusilalamike kombe la Mapinduzi halibaki nyumbani,”alisema Badru.

Issa Lambo aliekuwa mchezaji wa klabu ya Small Simba alisema ni jambo la aibu kuwa timu za Zanzibar, zinatolewa katika hatua ya mwanzo ya mashindano ambayo yanafanyika ndani ya visiwa hivyo na wenyeji. 

Lambo alisema timu za Zanzibar haziko makini katika ushiriki wao wa kombe hilo tofauti na timu za Tanzania Bara, ambazo hujipanga kikamilifu kwa ajili ya kushindana na kuchukua kombe.

“Tusilisema vibaya Shirikisho la Soka Zanzibar ZFF kwa kuwa haliwandai vizuri wachezaji, wao wenyewe ndio wanajiachia wanaenda kwenye mashindano makubwa wanafanya kama wanacheza mechi za kirafiki,”alisema Lambo.

Ramadhan Abdulrahman (Madundo) alisema timu za Zanzibar hazifanyi vizuri kwa  sababu kuu tatu, ambapo moja ni ligi kukosa ushindani.

Madundo aliitaja sababu nyengine ambayo inazifanya timu za hapa nyumbani kutofanya vizuri kwenye kombe la Mapinduzi, ni  kutokuwa na maandalizi ya kutosha ya mashindano.

Pia alisema viwango vya wachezaji wa Zanzibar viko chini na alifafanua kwamba ili soka liweze kupanda ni vyema wachezaji kuhakikisha wanajitahidi kufanya mazoezi .

“Tuna sababu nyingi zinazofanya kombe la Mapinduzi miaka yote livuke maji na lisibakia hapa nyumbani, na miongoni mwao ni hizo nilizozitaja hapo mwanzoni kwa hiyo ili timu zetu ziweze kuwa mabingwa, lazima wajitahidi na kusikiliza mawazo ya makocha ,”alisema Madundo.

Salum Riyami kocha  wa soka nchini Oman anasema kwamba bado wachezaji wa Zanzibar wanahitaji kunolewa zaidi katika kufanya vizuri na kuchukua ubingwa kwenye mashindano mbali mbali.

Riyami amesema kwamba dharau inayofanywa na wachezaji kwa kuyaona mashindano ya kombe la Mapinduzi ni sawa na mechi za kirafiki ndio inayochangia kutofanya vizuri na kombe kwenda timu nyengine.

“Vijana hawataki kusikiliza walimu wao wanaona wakicheza na Yanga au Simba ni sawa na mechi za kirafiki, wakati sisi tilipokuwa tunacheza ligi tu tukifungwa tunaumia na tunafanya juhudi ili mechi inayofuta tuwafunge,”alisema Riyami.

Saleh Juma kocha wa timu ya Puling Land amesema ni wajibu wa kila mtu kuhakikisha wanashirikiana, ili timu za nyumbani zifanye vyema katika mashindano hayo na hatimae kuchukua ubingwa.

Kocha huyo alisema sio wakati wa kuanza kulaumiana au kulaumu wachezaji, ni  vyema kuhakikisha nini kinafanyika ili kujua tatizo lipate kutafutiwa ufumbuzi.

“Tuache lawama tatizo lipo tena lishakuwa la siku nyingi na hivi sasa tumeweka mazoea kwamba Azam,Simba ,Yanga,Mtibwa  ndo mabingwa wa kombe hilo sisi tunaenda kushiriki na kutolewa njiani,”.

“Ni vizuri tukashirikiana na klabu zote za soka nchini pamoja na wadau ili kujua tatizo liko wapi tuweze kulitatua na tupate mafanikio, naamini tukifanya hivyo kombe la Mapinduzi litabakia nyumbani kila mwaka,”alifafanua.