NA ZAINAB ATUPAE

MSEMAJI wa timu ya Kundemba FC inayoshiriki  ligi daraja la pili mkoa Mjini Ali Said ,amesema watahakikisha wanafanya vyema na kushinda  mechi zilizobaki,ili kujiweka katika nafasi nzuri.

Ali aliyasema hayo juzi wakati alipokuwa akizungumzia  malengo ya timu yao katika kipindi hiki ambacho michezo imezuiliwa na serikali kutokana ugonjwa wa virusi vya corona.

Alisema hadi sasa wamebaki mechi nne,lakini wana imani watashinda mechi hizo kwani wamejipanga ingawa hawafanyi mazoezi ya pamoja.

Alisema timu yao iko vizuri wanachosubiri ni serikali kutangaza  ligi nyengine kuendelea,ili kuendelea na mashindano yao.

Aidha waliwataka wachezaji  kuendelea kufanya mazoezi kama walivyopangiwa na uongozi wa timu,ili kujiandaa kumaliza mechi zilizobakia.

Hivyo waliwataka wadau na wapenzi wa timu hiyo kuzidia kuwaunga mkono kumaliza mechi zao ndani ya msimu huu.

Kundemba  inaendelea kushika nafasi ya nane katika msimamo wa ligi hiyo kwa pointi 27 ambapo nafasi ya kwanza inashikiliwa na timu ya Gulioni FC yenye pointi 46 nafasi ya pili timu ya Gulioni City yenye pointi 44.