Mbivu, mbichi kujulikana leo

NA HUSNA MOHAMMED

JUMLA ya wagombea 206 wa viti maalumu wanawake waliojitokeza kuwania nafasi za Ubunge na Uwakilishi kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar wataingia katika kinyanganyiro cha kutafuta nafasi ya kuwania nafasi hizo katika uchaguzi mkuu wa 2020.

Kati ya wagombea hao 206, viti vya Baraza la Wawakilishi vinagombewa na watu 118 huku nafasi za Ubunge zikiwa na wagombea 91 ambapo uchaguzi wao unafanyika leo Tanzania nzima ikiwa ni hatua ya awali ya mchujo wa wagombea hao.

Akizungumza na gazeti hili, Naibu Katibu Mkuu Umoja wa Wanawake Tanzania Zanzibar (UWT), Tunu Juma Kondo alizitaja nafasi zinazogombaniwa ni pamoja na viti maalumu, nafasi za watu wenye ulemavu na nafasi za wasomi.

Nafasi nyengine ni nafasi za jumuiya zisizo za kiserikali na nafasi za jumuiya ya wafanyakazi na kufafanua kuwa nafasi hizo wanaogombea kupitia viti maalumu kwa uwakilishi ni 87 huku ubunge ni nafasi 59.

Tunu pia alizitaja nafasi za kupitia watu wenye ulemavu kwa nafasi za ubunge 13 ambapo uwakilishi jumla ya wanawake 15 wamejitokeza kugombea nafasi hizo.

Sambamba na hilo alizitaja nafasi za ubunge kwa jumuiya zisizo za kiserikali (NGOs) ni 12 ambapo kwa uwakilishi hakuna wagombea.

Kwa upande wa nafasi za wasomi kwa nafasi za ubunge Tunu alizitaja kuwa ni wagombea watano wamejitokeza ambapo kwa uwakilishi jumla ya nafasi 16 wamejitokeza katika kinyang’anyiro hicho.

Akizungumzia kuhusiana na mchujo huo alisema kuwa wagombea watakaokidhi vigezo ndio watakaoteuliwa ikiwa ni pamoja na watakaopata kura nyingi.

“Kwa mara ya kwanza wanawake wamehamasika kujitokeza kwa wingi katika nafasi hizi, kuna kinyang’anyiro cha kutosha, malalamiko hayana nafasi kwa uteuzi huo kwani wenye kura nyingi ndio watakaoteuliwa na baadae kufuatia uteuzi mwengine Dodoma,” alisema.