MUNICH, Ujerumani

MFUNGAJI bora wa  Bundesliga  Robert Lewandowski  wa  mabingwa Bayern Munich, amechaguliwa  kuwa  mchezaji  bora  uwanjani  kwa msimu  huu  na  wachezaji  wa  ligi , katika  kura  iliyoendeshwa  na jarida la  mchezo  la  Kicker.

Kicker  limesema  raia  huyo  wa Poland Lewandowski  alipata  asilimia 42.6 ya  kura  kutoka wachezaji  wa  ligi ya  kwanza 270  na  kuongoza  dhidi  ya mshambuliaji  wa  Borussia  Dortmund Jadon Sancho aliyepata asilimia  14.1  na  mchezaji  wa  kiungo  wa Bayern Munich Joshua Kimmich.

Lewandowski  alipachika  wavuni  mabao 34 na  kuwa  mfungaji bora  wa  Bundesliga kwa  mara ya  tano  katika muda wake  wa kucheza kandanda. Ana  magoli 55  katika  mashindano  yote msimu huu, kiasi ambacho kinaweza  kuwa  bora  zaidi  wakati  Champions League ikianza  tena mwezi  ujao.