MNAMO mwaka 2011 wakati wa vuguvugu la mabadiliko katika mataifa ya kiarabu, ulipoanza upinzani dhidi ya Muammar Gaddafi nchini Libya, mataifa kama Ufaransa yakaona hiyo ndio fursa pekee ya kuiingilia vitani nchini humo.

Kuingilia kati kwa NATO katika bita hivyo kukasababisha utawala wa Libya uliokuwa katika mji wa Tripoli ukaangushwa na vita vilipopamba moto, Muammar Gaddafi naye akauawa.

Kama ilivyo katika mifano mingine kwa namna moja au nyingine utulivu wa kisiasa, kijeshi na kiuchumi ukashindwa kupatikana nchini Libya baada ya mataifa ya magharibu kumuangusha Muammar Gaddafi.

Kwa bahati mbaya mataifa ya magharibi yalijua kumuangusha tu Muammar Gaddafi lakini hayakufikiria kumuweka mbadala ambaye ataleta ulivu wa kisiasa nchini Libya.

Inavyosemekana utajiri wa nishati wa nchi hiyo na eneo la kijiografia la kimkakati kaskazini mwa Afrika ukasababisha mataifa mengi kulimezea mate na ili waweze kufanikiwa lazima Muammar Gaddafi aondolwe madarakani.

Kinachoshuhudiwa hivi sasa nchini Libya ni vuru na vita visivyokwisha ambapo kwa kiasi fulani vinachangiwa na mataifa ya nje ambayo kila moja linapendelea upende mwengine kwa maslahi yao.

Mataifa yaliyofikiri kwamba serikali halali ya maridhiano ya kitaifa inayotambuliwa na Umoja wa Mataifa haitajali maslahi yao ukianzia na Umoja wa Falme za Kiarabu, Misri na Ufaransa yakataka kumuweka madarakani jenerali Hafter ambaye alikuwa katika juhudi za kufanya mapinduzi ya serikali kwa kumuunga mkono.

Hilo liliposhindikana   huko Tobruk walifuata utawala wa nakisi chini ya uongozi wa Jenerali Haftar na waliunga mkono utawala mbadala wa Tripoli na kuchukua udhibiti wa miji kama Mistara na Sirte.

Saudi Arabia pamoja na Umoja wa Falme za Kiarabu wakamshawishi Rais Trump naye amuunge mkono Haftar. Pamoja na ushirika huo kumsaidia Haftar kwa kila nyenzo na hata kuingia katika uwanja wa mapambano, walishindwa kuudhibiti mji wa Tripoli.

Mazungumzo mengi ya amani yalipendekezwa na kuzikutanisha pande zinazopingana nchini Libya, lakini bado hali ya machafuko inaendelea, katika hatua hii Umoja wa Mataifa unasemaje.

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Gutteres hivi karibuni ameonya alipokuwa akizungumza katika baraza la usalama kwa kueleza kwamba mzozo wa Libya umeingia katika awamu mpya ambapo uingiliaji kati wa kigeni umefikia viwango ambavyo havijapata kushuhudiwa.

Kwenye kikao hicho kilichohudhuriwa pia na mawaziri wa mambo ya nje kilichofanyika kwa njia ya kwa njia ya video, Gutterres, alisema hakuna tena muda huko Libya, ambako uingiliaji kati kutoka nchi za nje umeongezeka kwa hali ya juu pamoja na kupelekwa kwa vifaa na silaha za kisasa pamoja na mamluki wanaoongezeka.

“Tuna wasi wasi mkubwa sana kutokana na kiwango cha kuimarishwa shughuli za kijeshi karibu na mji wa Sirte na kiwango cha juu cha uingiliaji kati kutoka nchi za nje katika mzozo huu, kwa kukiuka vikwazo vya Umoja wa Mataifa na ahadi zilizotolewa Berlin na mataifa wanachama wa baraza hili la usalama.”

Gutterres aliendelea kusema kwamba licha ya kuongezeka kwa mivutano Umoja wa Mataifa umeendelea kujadiliana na pande zote ili kuzuia vita kuenea katika jimbo la Sirte lenye utajiri wa mafuta ambalo linazalisha asilimia 60 ya mapato ya mafuta ya nchi hiyo.

Wapiganaji wa serikali ya GNA inayotambuliwa na UN walionekana wakitayarisha silaha zao kabla ya kuelekea mji wa Sirte kutokea magharibi huku wapiganaji wa mashariki wakijitayarisha pia.

Mji huo umegeuka haraka kuwa mstari wa mbele katika vita hivyo baada ya wanajeshi wa serikali ya Tripoli wakisaidiwa na Uturuki kuwarudisha nyuma wapiganaji wa jeshi la taifa la Libya LNA kutoka Tripoli na maeneo ya kaskazini magharibi ambako wamekuwepo tangu mwezi April 2019.

Jeshi la LNA linaloongozwa na jenerali muasi Khalifa Haftar linaloungwa mkono na Umoja wa Falme za Kiarabu, Urusi, na Misri limepata pigo kubwa hivi karibuni kwa kurudishwa nyuma hadi mji huo wa Sirte.

Jeshi la serikali lilizuiliwa karibu na Sirte kutokana na mashambulizi ya ndege zisizojulikana zimeokea wapi mwishoni mwa wiki iliyopita. Msemaji wa jeshi la serikali, Mohamed Qanunu, alisema mapema kwamba wao hawapendelei vita.

“Sisi hatukuanzisha vita. Sisi hatuanzishi vita kwa vile tunapenda kuua au kuuliwa, lakini tunabidi kupigana ili kukomboa miji kutoka kwa wanamgambo na makundi ya uhalifu. Ikiwa hili linaweza kufanyika kwa amani sisi tuko tayari.”

Juhudi kubwa za kidiplomasia zinaendelea kati ya mataifa yanaohusika katika vita hivyo ili kutafuta njia za kumaliza mzozo kwa mazungumzo. Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Heiko Maas kwa pande wake anatoa wito wa majadiliano kuanza tena.

Heiko Maas, Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Ujerumani anasema: “Itakuwa jambo zuri ikiwa matatizo yaliyopo yanaweza kutanzuliwa kwa majadiliano, na hilo linaweza kufanyika kwa njia ya mazungumzo ya dhati, wazi, na tunatumaini jambo hilo litafanyika katika siku chache zijazo.”

Mwishoni mwa wiki wakazi wa mji wa Benghazi waliandamana dhidi ya uingiliaji kati wa Uturuki katika mambo ya ndani ya nchi yao.

Libya imekuwa katika hali ya ghasia tangu 2011 baada ya kupinduliwa kwa kiongozi wa muda mrefu Muammar Ghaddafi na tangu 2015 imegawika kati ya serikali ya GNA na LNA ya mashariki.

Juhudi za UN kutafuta suluhisho la amani hadi hivi sasa hazijafanikiwa na wachambuzi wanasema njia pekee ni kwa Uturuki na Rashia kufikia makubaliano kumaliza mzozo huo wa Libya.