TRIPOLI, LIBYA

OFISA mmoja wa jeshi amesema serikali ya Libya inayotambulika kimataifa inakusanya vikosi vyake kwa mapambano yanayokaribia ya kuuteka mji wa Sirte kutoka katika kikosi hasimu cha mbabe wa kivita Khalifa Haftar.

Msemaji wa vikosi vinavyofungamana na serikali ya Libya Mostafa al-Majai alisema kwamba jeshi linaloundwa na serikali hiyo ni kubwa mno.

Al-Majai pia alisema mapigano hayo pia yatalenga kuviteka visima vya mafuta vilivyo chini ya udhibiti wa vikosi vya Haftar.

Jeshi la Haftar lililoko mashariki mwa Libya bado halijatoa tamko kuhusiana na suala hilo.

Vikosi vya Haftar viliudhibiti mji wa Sirte tangu mwezi Januari. Mji huo wa pwani ni lango kuu la kuingia na kutoka katika visima vikuu vya mafuta vilivyoko mashariki mwa nchi hiyo.

Wapiganaji wa serikali ya Libya katika wiki za hivi karibuni walifanikiwa kudhibiti maeneo kadhaa karibu na mji mkuu Tripoli.