YERUSALEMU,ISRAEL

WANANCHI wa Ubelgiji wamefanya maandamano ya kulaani na kupinga mpango wa utawala wa Israel wa kutaka kuteka ardhi zaidi za Wapalestina katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan.

Kwa mujibu wa shirika la habari la Anadolu la Uturuki, mamia ya waandamanaji walishiriki kwenye maandamano hayo kupinga mpango wa kidhulma wa utawala wa Israel wa kutaka kupora ardhi zaidi za Wapalestina katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan na kuziunganisha na radhi nyengine za Wapalestina zinazokaliwa kwa mabavu na Waisrael ambazo zimepachikwa jina bandia la Israel. 

Maandamano hayo yalifanyika katika mji mkuu wa Ubelgiji, Brussels,ambapo Waandamanaji walibeba mabango yenye maneno “Tunapinga kutekwa ardhi zaidi za Wapalestina,””Palestina inateseka” na “Simama imara Palestina” katika kupinga vikali ugaidi huo wa utawala wa Israel.

Kabla ya hapo pia, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres alizungumza katika mkutano kwa njia ya video katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na kuutaka utawala huo uachane na mpango wake wa kupora ardhi zaidi za Wapalestina katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan.

Viongozi na makundi yote ya Palestina yaliungana na sasa hivi yako kitu kimoja katika kukabiliana na njama hizo za utawala wa Israel ambazo ni sehemu ya mpango wa kivamizi na kidhalimu wa Marekani uliopachikwa jina la “Muamala wa Karne.” 

Kwa mujibu wa mpango huo wa Marekani, mji wa Quds Tukufu ambao una Kibla cha Kwanza cha Waislamu yaani Msikiti wa al Aqsa, utakabidhiwa kwa utawala wa Israel.