BERLIN,UJERUMANI
WAZIRI wa mambo ya nje wa Ujerumani Heiko Maas amesema haoni uwezekano wa Urusi kurudishwa katika kundi la mataifa yenye nguvu za kiuchumi duniani, kufuatia pendekezo la Rais wa Marekani Donald Trump.
Ujerumani ilikataa ombi lililowasilishwa na Rais Donald Trump wa Marekani la kutaka Urusi irudishwe katika kundi la mataifa saba yenye uwezo mkubwa wa kiuchumi duniani .
Alisema Waziri huyo katika mahojiano yaliyochapishwa katika gazeti la Rheinische Post.
“Sababu ya Urusi kutolewa katika kundi la G7 ni uingiliaji wake katika eneo la Mashariki mwa Ukraine, na kuiteka rasi ya Crimea. Kama bado hakujapatikana suluhu huko,sioni nafasi ya kuiruhusu tena Urusi ndani ya kundi hilo”, alisema Maas.
Urusi iliondolewa kutoka kundi la mataifa saba mwaka 2014 baada za Moscow kuiteka rasi ya Crimea kutoka Ukraine.
Trump alipendekeza upanuzi wa nchi za kundi hilo na tayari alisema anapanga kuzialika Australia, India, Urusi na Korea Kusini kwa mkutano unaofuata ambao anapanga kuwa mwenyeji mnamo mwezi Septemba.
Kundi la mataifa Saba lilikuja pamoja mwaka 1975 kama mataifa saba muhimu yaliyoendelea zaidi kiviwanda wakati huo.
Nchi wanachama wa G7 ni Uingereza, Canada, Ufaransa, Ujerumani, Italia, Japan na Marekani mwaka 1998 Urusi iliongezwa kwenye kundi hilo na kuwa G8 lakini baadaye iliondolewa.
Maas alisema uhusiano na Urusi kwa wakati huu ni mgumu katika kila sehemu,pia aliikosoa Urusi kwa kuzuia kupelekwa misaada ya kibinadamu kwa kiasi ya watu milioni 1.5 nchini Syria.
Waziri huyo aliitolea wito Urusi kuongeza juhudi za kumaliza mzozo mashariki mwa Ukraine, Syria na Libya.