KINSHASA,DRC

WATU  zaidi ya 30 wameuwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na mamia kuyakimbia makaazi yao baada ya kutokea mapigano kati ya wapiganaji wa kundi la waasi wa NDC katika Wilaya ya Walikale, mashariki mwa nchi hiyo.

Kwa mujibu wa taarifa  za usalama mauaji hayo yalitokea katika siku za hivi karibuni huku ukosefu wa usalama katika maeneo hayo ya mashariki mwa DRC ukiendelea kuwa tatizo kubwa katika maeneo hayo.

Wakati huo huo wanajeshi watatu wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo waliuawa, mmoja akijeruhiwa vibaya baada ya waasi wa kundi la M23 kushambulia eneo la Rutshuru, karibu na Hifadhi ya wanyama ya virunga, katika mkoa wa Kivu Kaskazini.

Kwa mjibu wa mamlaka ya eneo hilo, mapigano makali yalishuhudiwa kwa muda kati ya jeshi la serikali, FARDC, na waasi hao wa M23.

Maeneo ya mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo yaliendelea kushuhudia ukosefu wa usalama huku raia wakivikosoa vyombo vya usalama kwa kushindwa kukabiliana na harakati za makundi ya waasi katika maeneo hayo.

Makundi yenye silaha yanaendelea kutekeleza vitendo viovu dhidi ya raia, hususan mauaji, ubakaji, na uporaji wa mali za wakaazi wa maeneo hayo.

Mikoa ya Ituri, Kivu Kaskazini na Kivu Kusini inaendelea kuwa ngome za harakati za makundi hayo na kusababisha maelfu ya watu kukimbia makaazi yao na kukimbilia katika maeneo salama.

Ripoti mbalimbali zinasema kuwa, eneo la mashariki mwa DRC limekuwa likishuhudia machafuko ya mara kwa mara baina ya makundi ya wanamgambo kwa upande mmoja na wanamgambo na maofisa usalama kwa upande mwengine, kutokana na kuwa na utajiri mkubwa wa madini hususan dhahabu na almasi.