NA MWANDISHI WETU, MASASI

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Pombe Magufuli na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein jana waliwaongoza Watanzania katika maziko ya aliekuwa Rais wa ya awamu ya tatu Benjamin Mkapa.

Maziko hayo yaliyofanyika katika kijiji cha Lupaso, wilaya ya Masasi mkoani Mtwara mahali alipozaliwa kiongozi huyo miaka 82 iliyopita, yalitanguliwa na ibada maalum ya kumuombea marehemu.

Mbali na marais hao, maziko hayo pia yalihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa chama, serikali na wananchi wa ndani na nje ya mkoa Mtwara huku akipigiwa mizinga 21 kama heshima ya kumuaga.

Akizungumza kabla ya mwili wa marehemu kushushwa kaburini, Dk. Magufuli alisema uamuzi wa kumzika Mzee Mkapa kijijini kwao kunatokana na maelekezo yake.

Alisema awali serikali ilitenga eneo kwa ajili ya mazishi ya viongozi wa kitaifa jijini Dodoma lakini alilazimika kulitoa kwa wananchi baada ya kiongozi huyo kuelekeza kuwa siku akifa akazikwe kijijini alikozaliwa.

“Nilimuuliza Mzee Mkapa kipindi yupo hai, Mzee unataka kuzikwa wapi pindi utakapofariki, alinijibu anataka kuzikwa kijijini kwao Lupaso, mkoani Mtwara. Mzee Kikwete nae alisema anataka kuzikwa kijini kwao Msoga, mkoani Pwani.

Aliongeza; “Niliogopa kumuuliza Mzee Mwinyi kwa sababu alikuwa na miaka 92, niliogopa kuona kama natabiri kifo chake, hata mimi nasema nikifariki nataka kuzikwa nyumbani Chato”.

Rais Magufuli alieleza kuwa Mzee Mkapa alikuwa na sehemu nyingi za kuzikwa lakini alichagua kuzikwa Lupaso kutokana na mapenzi yake kwa watu wake jambo ambalo ni funzo muhimu linaloachwa na marehemu.

“Angependa angezikwa sehemu yoyote, Dar es Salaam au Lushoto, ana maeneo makubwa tu lakini alisema anataka kuletwa Masasi na hii ni kutokana na jinsi anavyokupenda kwao na watu wake”, alisema Magufuli.


Aidha Dk. Magufuli aliishukuru kamati ya maandalizi ya mazishi iliyoongozwa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa Majaliwa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi, Wananchi, viongozi wa dini zote sambamba na vyombo vya ulinzi na usalama kwa kushiriki bega kwa bega kuhakikisha safari ya mwisho ya hayati Mzee Mkapa katika makazi yake ya milele inakamilika kwa heshima.