KARA,UTURUKI

MAHAKAMA moja nchini Uturuki imesikiliza kesi ya maofisa 20 wa Saudi Arabia walioshtakiwa kwa mauaji ya Jamal Khashoggi, mwandishi wa habari raia wa nchi hiyo.

Maofisa wa ofisi ya mwendesha mashitaka mjini Istanbul walivieleza vyombo vya habari kuwa,kesi hiyo ilitakiwa kuanza kusikilizwa jana Uturuki katika mahakama kubwa ya wilaya ya Caglayan iliyoko kwenye mkoa huo wa Instanbul.

Khashoggi, mwandishi wa makala katika gazeti la Washington Post ambaye alikuwa na umri wa miaka 55, aliuliwa ndani ya ubalozi mdogo wa Saudi Arabia mjini Instanbul Oktoba Pili 2018 baada ya kuingia ubalozini humo alikokwenda kuchukua waraka wa kibali kwa ajili ya mpango wake wa kufunga ndoa.

Maofisa wa Uturuki walisema mwili wa Khashoggi ulikatwa vipande vipande ndani ya ubalozi huo wa Saudia na watu waliomuua,na mabaki ya kiwiliwili chake hayajapatikana hadi leo.

Mwezi Machi mwaka huu, waendesha mashitaka wa Uturuki waliwafungulia mashitaka raia 20 wa Saudi Arabia kwa kuhusika na mauaji ya Jamal Khashoggi,wakiwemo wasaidizi waandamizi wawili wa zamani wa mrithi wa ufalme wa nchi hiyo Mohammad bin Salman, ambaye kiuhalisia ndiye mtawala wa nchi hiyo hivi sasa.

Kwa mujibu wa hati ya mashitaka,Naibu mkuu wa zamani wa idara ya intelijensia ya Saudi Arabia Ahmed al-Assiri anakabiliwa na shitaka la kuunda kikosi cha mauaji na kupanga mauaji ya mwandishi huyo wa habari aliyekuwa mkosoaji mkubwa wa utawala wa Aal Saud.

Mshauri wa zamani wa mahakama ya kifalme na masuala ya vyombo vya habari Saud al-Qahtani, yeye alishitakiwa kwa kuchochea na kuongoza operesheni kwa kutoa amri na maagizo kwa kikosi hicho cha mauaji.

Washitakiwa wengine katika kesi hiyo ya mauaji ya Jamal Khashoggi ni maofisa wa Saudia ambao wanadaiwa kushiriki katika utekelezaji wa operesheni ya mauaji hayo.

Waendesha mashitaka wa Uturuki wameshatoa waranti wa kukamatwa washtakiwa hao.