LONDON,UINGEREZA

CHANJO ya virusi vya Corona inayofanyiwa uchunguzi na wanasayansi wa chuo kikuu cha Oxford nchini Uingereza inaonyesha kwamba ina nguvu za kuongeza nguvu ya kinga mwilini, kulingana na majaribio ya utafiti wa hatua za awali.

Matokeo yaliyochapishwa katika jarida la madawa la Uingereza, The Lancet, yalionyesha chanjo inayofanyiwa majaribio na kampuni ya madawa ya Astra-Zeneca na chuo kikuu cha OXFORD, ilitoa majibu mazuri kwenye seli zinazopambana na maradhi Pamoja na seli muhimu kwenye mfumo wa kinga zijulikanazo kama T-cells.

Majaribio hayo ni sehemu ya hatua ya pili ya uchunguzi wa chuo cha Oxford, ambao haukuangalia iwapo chanjo inazuia dhidi ya maambukizi ya virusi vya Corona, swali ambalo litajibiwa kwenye hatua ya tatu ya majaribio ambayo tayari imeshaanza.

Utafiti unahitajika zaidi ili kubaini iwapo chanjo hiyo inatoa kinga kamili kwa mtu aliyeambukizwa virusi vya Corona, na iwapo inatoa kinga, ni kwa muda gani, alisema Andrew Pollard, ambaye alitayarisha ripoti kuhusu utafiti wa chuo cha Oxford.