NA WAANDISHI WETU

ZOEZI la uchukuaji wa fomu kuwania nafasi za uwakilishi na ubunge kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM), linazidi kunoga baada ya idadi ya wagombea kuoengezeka katika wilaya za Unguja na Pemba.

Zoezi hilo ambalo ni la siku nne liloanza Julai 14 Tanzania nzima ambapo linatarajiwa kumaliza Julai 17 majira ya saa 10 jioni.

Kwa upande wa wilaya ya Kaskazini ‘A’ Unguja, jumla ya wagombea 57, nafasi ya uwakilishi 29 na ubunge ni 28 huku wanawake wakiwa wawili kwa nafasi ya ubunge.

Waliochukua fomu kwa upande wa wilaya ya Kaskazini ‘A’ Unguja ni Nadir Abul-latif anaetetea kiti chake cha uwakilishi wa jimbo la Chaani, Juma Othman Hija jimbo la Tumbatu na Ali Khamis Makame wa kuchukua fomu ya kuwania uwakilishi jimbo la Mkwajuni.

Akizungumza na waandishi wa habari aliyekuwa mwakilishi wa jimbo la Chaani, Nadri Abdul-latif aliyefika majira ya saa 3:00, alisema amechukua fomu kwa mara nyengine baada ya kujiona ana kigezo cha kuendelea kuliongoza jimbo la Chaani.

Nae aliyekuwa mbunge wa jimbo la Tumbatu, Juma Othman Hija, alisema, alifikia maamuzi ya kuchukua fomu hiyo, baada ya kujiona kuwa ana kila kigezo cha kuendelea tena kuwatumikia wananchi wa jimbo hilo.

Akizungumza na Zanzibar Leo, mara baada ya kuwakabidhi fomu hizo, Katibu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Kaskazini ‘A’, Haji Machano, alisema, wanaCCM wengi wamejitokeza kuomba nafasi mbalimbali za uongozi.

WILAYA YA AMANI

Idadi ya waliochukua ni 54 ambapo nafasi ya uwakilishi walikuwa 29 na nafasi ya Ubunge 26 wakiwemo wanawake sita (uwakilishi) na ubunge wanawake saba.

WILAYA YA DIMANI KICHAMA

Makada waliojitokeza jumla ni 86 wakiwemo wanawake saba, ambao watatu walichukuwa fomu ya uwakilishi na wanne nafasi ya ubunge.

Katika wilaya hiyo jana waliojitokeza kuchukuwa fomu walifikia 57 ambapo kufatia idadi hiyo wamefikia 143 hadi jana.

WILAYA YA KATI

Waliojitokeza katika zoezi hilo kwa jana walikuwa jumla ya makada 32 wakiwemo wanawake sita na wanaume 26 kwa nafasi ya uwakilishi na Ubunge.

Katibu wa CCM, wilaya ya kati, Omar Justas, alisema kati ya wagombea hao wapo wakongwe ambao wanatetea nafasi zao akiwemo Mohamed Seif Khatibu (Ubunge) na Uwakilishi Mohamed Raza.

WILAYA YA KASKAZINI ‘A’

Kwa upande wa Wilaya ya Kaskazini ‘A’ Unguja, jana walikuwa jumla ya wagombea 57, nafasi ya Uwakilishi walikuwa ni 29 na Ubunge ni 28 huku wanawake wakiwa wawili kwa nafasi ya Ubunge.

WILAYA YA MKOANI

Katika wilaya hiyo jumla ya watia nia ambao walijitokeza kuchukuwa fomu wote kwa nafasi za ubunge na uwakilishi ni 36, ubunge 22 na 14 uwakilishi, huku wanawake wakiwa ni wanne wawili kwa kila upande.

Habari hii imeandaliwa na NA MADINA ISSA NA ABOUD MAHMOUD