NA WAANDISHI WETU

WAKATI Chama cha Mapinduzi (CCM) hapo jana kimefungua pazia kwa wanachama wake kuchukua fomu kwa ajili ya ubunge na uwakilishi na udiwani, makada wa chama hicho wamefurika kuchukua fomu kuwania nafasi hizo.

Katika wilaya ya Mjini hadi majira ya saa 10 alaasiri jumla ya makada zaidi ya 47 wamejitokeza kuchukua fomu ambapo wengi wao ni vijana.

Akizungumza na Zanzibar Leo katibu wa CCM wilaya ya Mjini Abdul-rahim Hamid alisema muamko wa uchukuaji fomu upo vizuri kwani tayari asilimia 80 ya makada wameshajitokeza kuchukua fomu katika majimbo manne ya wilaya hiyo.

Aidha alisema tayari majimbo hayo yameshapata watu ambao wameomba kuteuliwa na CCM katika kugombea majimbo hayo ikiwemo Jimbo la Malindi, Kwahani, Kikwajuni na jimbo la Jang’ombe.

Akizungumzia ushiriki wa wanawake katika kugombea nafasi hizo, alisema upo vizuri kwani tayari jumla ya wanawake tisa wameshajitokeza katika zoezi hilo.

“Katika zoezi hili tumeona muamko mkubwa upo kwa vijana ambao wamejitokeza kwa wingi kuchukua fomu ikiachia rika la wazee watatu tu mpaka sasa ndio waliojitokeza”, alisema.

Alisema, upo uwezekano mkubwa kuongezeka kwa wagombea hao katika siku zinazoendelea za zoezi hilo.

Mbali na hayo, alifahamisha kuwa, hadi sasa hakuna mwanachama aliyekosa sifa ya kuchukua fomu ikiwemo kuwa na kadi ya chama ambayo imesajiliwa kwa mfumo wa kielektroniki.

Mtia nia Mohamed Ahmada Salum akizumgumza mara baada ya kuchukua fomu ya kugombea nafasi ya Uwakilishi jimbo la Malindi, alisema ameamua kurudi tena katika jimbo hilo na imani yake maendeleo aliyoyafanya katika jimbo hilo wananchi watampa ridhaa ili aweze kufanya kazi na rais anaekuja katika kuwaletea maendeleo wananchi.

Naye mwanamama Ngaza Rashid Khamis aliyechukua fomu ya Ubunge jimbo la Kwahani, alisema ni matumaini yake kwamba uchaguzi utafanyika kwa amani na utulivu na yeyote ambae atateuliwa na chama basi watamuunga mkono kwa maslahi ya chama na wananchi kwa ujumla.

WILAYA YA KATI

Kwa upande wa wilaya ya Kati Unguja tayari watia nia 29 wamejitokeza kuchukua fomu za kugombea nafasi za Ubunge, Uwakilishi wakiwemo wanawake watatu kwa majimbo matatu yaliyokuwemo ndani ya wilaya hiyo.

Akizungumza na Zanzibar Leo, Katibu wa CCM wilaya ya Kati, Omar Justas, alisema zoezi hilo limekwenda vizuri kwani vijana na wanawake wamehamasika kujitokeza kwa wingi katika zoezi hilo.   

WILAYA YA MKOANI PEMBA

Aidha katika wilaya ya Mkoani jumla ya wanachama waliochukua fomu wamefikia 18 kwa Ubunge na Uwakilishi.

Akizungumza na Zanzibar Leo Katibu wa CCM wilaya ya Mkoani Mohamed Ali Abdalla, alisema zoezi hilo limekwenda vizuri kwani tayari jumla ya wanaCCM 11 wamejitokeza kuchukua fomu za kugombea Ubunge na saba wamechukua fomu za kugombea nafasi ya Uwakilishi katika majimbo manne ya wilaya hiyo wakiwemo vijana na wanawake.

WILAYA YA AMANI

Kwa upande wa wilaya ya Amani jumla ya wanaCCM 29 wamejitokeza kuchukua fomu za kugombea Ubunge na Uwakilishi wakiwemo wanawake wanne na wanaume 25 huku vijana wakifikia asilimia 70.

Aidha katika nafasi hizo wamejitokeza wakongwe ambao wanatetea nafasi zao akiwemo aliyekuwa mbunge wa Jimbo la Mpendae Salim Turkey, aliyekuwa mwakilishi wa jimbo hilo Mohammed Said Dimwa na aliyekuwa mwakilishi wa Jimbo la Magomeni Rashid Makame Shamsi.

Katibu wa CCM wilaya ya Amani, Ashraf Saleh Zungo, alisema zoezi hilo limekwenda vizuri na hakuna changamoto iliyojitokeza na wajumbe wote wamefuata taratibu zote ambazo zilielekezwa na chama.

WILAYA YA DIMANI

Kwa upande wa wilaya ya Dimani waliojitokeza kuchukua fomu za kugombea nafasi ya ubunge na uwakilishi ni 57 wakiwemo wanawake na vijana.      

Zoezi la uchukuaji wa fomu limeanza rasmi jana katika wilaya zote za CCM kwa nafasi ya Uwakilishi na Ubunge na kumalizika rasmi Julai 17.

WILAYA YA KASKAZINI ‘A’

Jumla ya wagembea 11 walijitokeza kuchukua fomu za ubunge na uwakilishi, ambapo wagombea saba wa nafasi za ubunge na wagombea wanne nafasi ya uwakilishi.

Katibu wa CCM Wilaya hiyo Haji Machano Juma alisema kati ya wagombea hao jimbo la Chaani walijitokeza wagombea sita likiongoza kuwa na wagombea wengi.

Katika nafasi hiyo waliochukua fomu ni Khamis Fumu Khamis kutoka Jimbo la Tumbatu na Ahmada Ali Ussi, Jimbo la Kijini  aliyejitokeza ni Nassor Haji Makame, Hassan Makungu Juma na Mohamed Ali Haji.

Kwa upande wa Jimbo la Chaani ni Khamis Kona Khamis, Ame Silima Khamis, Ali Ussi Ali, Hassan Vuai Hassan na Ali Haji Khamis. Nalo Jimbo la Mkwajuni waliojitokeza ni Jadi Simai Jadi.

Kwa upande wa nafasi ya uwakilishi waliojitokeza ni Sheha Makame Mussa na Mtumwa Mjomba Abdalla na Nizar Mohamed Juma ambao wanatokea Jimbo la Mkwajuni.

Jimbo la Nungwi Abdalla Abass Wadi na Jimbo la Chaani Haji Sheha Hamdu.

Habari hii imeandikwa na Khamisuu Abdallah, Mwajuma Juma, Aboud Mahmoud na Tatu Makame.