LONDON, England

INAELEZWA kuwa Manchester United inayonolewa na kocha mkuu, Ole Gunnar Solkjaer ipo kwenye hesabu za kuinasa saini ya kinda anayekipiga ndani ya Manchester City, Charlie McNeill.

Nyota huyo raia wa England anayekipiga ndani ya timu ya vijana ya Taifa anatajwa kuondoka ndani ya kikosi cha City msimu ujao, ambapo amedumu kwa miaka sita kwenye kituo cha kukuzia vipaji ndani ya City.

McNeill kupitia ukurasa wake wa Instagram aliandika kuwa anashukuru kwa ushirikiano  mkubwa aliyopata ndani ya miaka sita ndani ya kikosi hicho huku akiwashukuru pia wachezaji wenzake pamoja na benchi la ufundi.

Manchester City wameonekana kukubali kumruhusu kinda huyo mwenye miaka 17 aweze kuondoka huku ikielezwa kuwa wapo kwenye mazungumzo ya makubaliano na United.

Timu nyingine ambazo zimeonyesha nia ya kupata saini ya mshambuliaji huyo ni pamoja na Wolves pamoja na Leeds United.