NA HAFSA GOLO

SHILINGI milioni 29.5 zinatarajiwa kutumika kwa ajili ya maandalizi ya viwanja vya kusherehekea Eid al Haji inayotarajiwa kuanza ijumaa wiki hii.

Ofisa Uhusiano wa Baraza la Manispaa Mjini, Seif Ali Seif alieleza hayo wakati akizungumza na gazeti hili ofisini kwake Malindi.

Alisema fedha hizo ni makadirio ya awali yaliyozingatia mahitaji na maombi ya wafanyabiashara wanaotarajia kufanya biashara katika viwanja vya sikukuu vya Mnazi Mmoja mjini Unguja.

Alisema baraza limetumia kiasi hicho cha fedha kwa ujenzi wa mashamiana ili kuimarisha mazingira ya viwanja hivyo kuwa bora na kuleta ustawi mzuri kwa wafanyabiashara na watu watakaofika katika viwanja vivyo.

Akizungumzia kodi ya mabanda hayo kwa wafanyabiashara walioomba kutumia viwanja hivyo, seif alisema kwa wafanyabiashara wa vitu vya kuchezea watoto watalipa shilingi 80,000 na wauzaji wa vyakula watalipa shilingi 70,000.

Kuhusu huduma ya umeme alisema, kutakuwa na namna mbili za malipo ambapo kila mfanyabiashara atalazimika kulipia shilingi 15,000 za awali zitakazokuwa kwa ajili ya taa na fedha nyengine zitalipwa kulingana na ukubwa wa matumizi ya mfanyabiashara.

“Wafanyabiashara wote ndani ya siku nne watatozwa shilingi 15,000 kwa malipo ya huduma ya taa mbali na wengine watalipa kati ya shilingi 20,000 na 40,000 kwa ajili ya matumizi mengine ya ziada kulingana na mahitaji yao,” alisema.

Naye Ofisa afya na mazingira wa Baraza hilo, Rajab Salum Rajab alisema, baraza litahakikisha linasimamia usafi wa mazingira ili kuvutia na kuwalinda watu watakaofika katika viwanja vya kusherehekea sikukuu.

Aidha alisema hatua hiyo itakwenda sambamba na upatikanaji wa huduma bora kwa wateja ambazo zitazingatia usalama na afya za watumiaji.

Akizungumzia ada iliyowekwa, mfanyabiashara Othman Juma alisema iwapo biashara zitafanyika kama ilivyozoeleka na wananchi wakajitokeza kwa wingi, gharama zilizopangwa ni nafuu na hazitoleta athari kwa biashara zao.

Sherehe za sikukuu ya Eid el Hajj zinaanza leo ulimwenguni kote baada ya kukamilika kwa ibada ya hija ambayo ni nguzo ya tano ya kiislamu ambapo kwa Zanzibar, swala na baraza la eid linatarajiwa kufanyika katika mkoa wa Kaskazini Unguja.