KAMPALA,UGANDA

SHIRIKA la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa (UNHCR) limesema, wakimbizi watatu kutoka Sudan Kusini wameuawa, sita kujeruhiwa na wengine mamia kupoteza makaazi katika mapambano ya kikabila yaliyotokea kwenye kambi ya wakimbizi ya Palorinya, wilayani Obongi, kaskazini magharibi mwa Uganda.

Taarifa iliyotolewa na UNHCR ilisema, mapambano hayo yalitokea tarehe 13 mwezi huu, kutokana na wizi wa mazao katika kijiji cha Dama, ambapo nyumba zaidi ya 280 zilichomwa moto.

Pia ilisema, ingawa mapambano hayo yalimalizika tokea wiki iliyopita, lakini hali ya mvutano bado inaendelea, na kuongeza kuwa watu 30 walikamatwa na wanashikiliwa katika kituo cha polisi cha Obongi.