WanaCCM wapokea kwa shangwe kubwa
Aahidi kutowaonea haya wabadhirifu, wala rushwa
Dk. Shein asema Mwinyi mzanzibari kindakindaki
MWINYINVUA NZUKWI NA KHAMISUU ABDALLAH
MGOMBEA Urais wa Zanzibar kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi (CCM) Dk. Hussein Mwinyi, amesema iwapo atapata ridhaa kuiongoza Zanzibar hatakuwa na muhali wala huruma kwa wala rushwa, wabadhilifu wa mali za umma na wazembe.
Kauli hiyo aliitoa jana wakati akizungumza na wanaCCM na wananchi wa Zanzibar baada ya kuwasili katika Ofisi kuu ya CCM Kisiwandui Zanzibar kwenye hafla maalum ya kutambulishwa rasmi baada ya kuchaguliwa na halmashauri kuu ya CCM taifa kuwa mgombe wa nafasi.
Alisema, wakati atakapokuwa anatekeleza mambo ya maendeleo kwa wananchi wa Zanzibar, hatokuwa tayari kuona watu wanashindwa kuwajibika na kuzorotesha mipango hiyo.
“Dk. Shein amewaambieni kwamba wengi wenu kiutendaji hamnitambui kwa sababu nimefanya kazi miaka 11 katika wizara ya ulinzi na mambo mengi tunafanya ndani, lakini nitaazima maneno ya Dk. John Pombe Magufuli kwamba ‘mtanielewa’,” alisema.
Alisema hana shaka na mapokezi aliyopata huku akiamini kuwa ni dalili za ushindi katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika baadae mwaka huu.
Dk. Mwinyi alisema endapo atachaguliwa kuwa rais wa Zanzibar atahakikisha anaendelea kuuenzi na kudumisha Mapinduzi ya Zanzibar kwa vitendo na muungano uliodumu kwa miaka mingi.
Aidha mgombea huyo alimpongeza Dk. Shein kwa kumfunza mambo mengi ikiwemo subira, uvumilivu na kukubali kupokea ushauri.
Dk. Mwinyi, alisema lengo lake ni kuendelea kuijenga nchi na kuleta maendeleo kuanzia pale alipoishia Dk. Shein hasa kwenye miradi ambayo haijakamilika pamoja na kusimamia miundombinu na huduma za jamii kwa ustawi wa wananchi wa Zanzibar.
Aidha aliwahakikishia wananchi wa Zanzibar kuwa amefanya maamuzi ya kugombea urais wa Zanzibar kwa nia ya kuwatumikia wazanzibari kwa nguvu zake zote na kuwaletea maendeleo.
Akimtambulisha mgombea huyo Makamu Mweyekiti wa CCM Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein, aliwataka wazanzibari kuwaapuza watu wanaosema kuwa Dk. Mwinyi sio mzaliwa wa Zanzibar na kwani wamefilisika kisiasa.
“Dk. Mwinyi sio mgeni nataka niwathibitishe wazanzibari kuwa huyu ni mwanakindakindaki wa Zanzibar, amezaliwa hapa na wazee wake wapo, wenye wasiwasi wakaulize sio waseme mambo wasioyajua,” alisema.