BAMAKO,MALI
MARAIS wanne wa nchi za Afrika Magharibi wamewasili Bamako mji mkuu wa Mali kwa lengo la kusuluhisha mzozo wa kisiasa kati ya vuguvugu la M5 na Rais wa nchi hiyo Ibrahim Boubacar Keita.
Ujumbe huo wa ngazi ya juu wa Jumjuiya ya Kiuchumi ya Nchi za magharibi mwa Afrika ECOWAS unaoundwa na Rais wa Niger Mahamadou Issoufou, Rais wa Senegal Macky Sall, Rais wa Ghana Nana Akufo-Addo na Rais wa Cote d’Ivoire Alassane Ouattara,uliwasili Bamako leo kwa lengo la kuzishawishi pande mbili zinazozona nchini humo kufikia mwafaka.
Hivi karibuni wapinzani nchini Mali walikataa pendekezo la Jumuiya ya Kiuchumi ya Nchi za magharibi mwa Afrika ECOWAS la kuundwa serikali ya umoja wa kitaifa nchini humo kama njia ya kuhitimisha mgogoro unaoikabili nchi hiyo.
Awali Rais Keita alikuwa ameafiki pendekezo la kuundwa serikali ya umoja wa kitaifa, kufanyiwa mabadiliko mahakama kuu na kuvunjwa bunge lakini wapinzani wamekuwa wakisisitiza kuwa mabadiliko hayo hayatoshi na wanamtaka aondoke madarakani.
Kuanzia Juni 10 Mali imekuwa ikishuhudiwa maandamano makubwa dhidi ya Rais Keita ambapo waandamanaji wanasisitiza kuwa lazima aondoke madarakani.
Wapinzani wanasema rais huyo amefeli katika utendaji kazi wake kuhusu mgogoro wa muda mrefu wa waasi, mgogoro wa kiuchumi na mvutano ulioibuka baada ya uchaguzi wa bunge mwaka jana.