WASHINGTON,MAREKANI

MAREKANI imerikodi tena maambukizi mapya ya juu zaidi ya virusi vya corona baada ya watu 67,632 kuthibitishwa kuambukizwa kwa siku moja.

Hayo ni kwa mujibu wa takwimu za chuo kikuu cha Johns Hopkins.

Tangu mwisho wa mwezi uliopita Marekani ilikuwa ikirikodi idadi ya juu ya maambukizi ya corona  kati ya watu 55,000 hadi 65,000 kila siku.

Hayo yanajiri wakati mkuu wa idara ya magonjwa ya kuambukiza nchini Marekani Antony Fauci akisema haelewi juhudi za baadhi ya maofisa wa ikulu ya rais kumdharau na anaamini hilo ni kosa kubwa.

Katika tukio jengine nchini Brazil rais wa nchi hiyo Jair Bolsonaro, alithibitishwa kuambukizwa tena virusi vya corona, lakini aliandika kwenye ukurasa wake wa Twitter kuwa yuko salama.

Brazil ni taifa la pili ambalo limeathiriwa zaidi na janga la corona baada ya Marekani, likiwa na takriban watu milioni mbili walioambukizwa na zaidi ya watu 75,000 wamefariki.