NA MWAJUMA JUMA

SHIRIKISHO la soka Zanzibar (ZFF) limesema linasubiri taarifa ya maandishi juu ya vurugu zinazodaiwa kufanywa na wapenzi na mashabiki wa timu ya Mlandege katika mchezo wao wa ligi kuu ya Zanzibar dhidi ya KMKM.

Mlandege ilidaiwa kufanya vurugu hizo na kuharibu baadhi ya vifaa vya uwanja wa Mao Zedong A, mara baada ya mchezo huo kumalizika kwa madai ya kuonewa na mwamuzi.

Katika mchezo huo ambao ulichezeshwa na mwamuzi Nassir Msomali ulimalizika kwa sare ya kufungana mabao 2-2.

Kaimu katibu wa shirikisho hilo Ali Ame Vuai akizungumza na mwandishi wa habari hizi, alisema hana taarifa yoyote aliyopokea kwa maandishi na  amesikia taarifa hizo kama ambavyo wengi wamezisikia.

“Mimi sina taarifa yoyote niliyopata mpaka sasa zaidi ya kusikia kama ambavyo wewe ulivyosikia”, alisema.