BURMA,MYANMAR

SHIRIKA  la kutetea haki za binadamu la Amnesty International limesema mashambulizi ya anga yaliyofanywa hivi karibuni na jeshi la Myanmar katika mkoa wa Rakhine na kuua idadi kubwa ya raia wakiwemo watoto wadogo ni jinai za kivita.

Katika ripoti mpya ilisema shirika hilo limelitaka Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lianzishe uchunguzi wa jinai za kivita dhidi ya wanajeshi wa Myanmar waliohusika na hujuma hizo za anga za Machi na Aprili mwaka huu.

Katika ripoti hiyo, Amnesty International ilisema imekusanya ushahidi mpya unaoonyesha kuwa jeshi la Myanmar linalofahamika kama Tatmadaw lilitekeleza mashambulizi ya anga na kuvishambulia kwa mabomu vijiji kadhaa vya majimbo ya Rakhine na Chin kati ya mwezi Machi na Aprili mwaka huu na kuua raia wengi wasio na hatia wakiwemo watoto wadogo.

Amnesty ilinukuu mashuhuda wa hujuma hizo wakisema watu tisa waliuawa katika mashambulizi ya anga ya Machi 14 na 15 dhidi ya mji wa Paletwa, akiwemo mtoto wa miaka saba.

Aidha raia wengine saba waliuawa katika hujuma nyengine ya anga ya Aprili 7 katika mji huo huo.

Kuanzia Oktoba 25 mwaka 2017, Jeshi la Myanmar likisaidiwa na Mabuddha wenye misimamo ya kufurutu ada, lilianzisha oparesheni ambayo ilipelekea zaidi ya Waislamu 6,000 kuuawa kwa umati na wengine zaidi ya milioni moja kukimbilia katika nchi jirani ya Bangladesh.

Baada ya kupita takribani miaka mitatu tokea Jeshi la Myanmar lianzishe hujuma na mauaji dhidi ya Waislamu nchini humo katika jimbo la Rakhine, bado taasisi za kimataifa hasa Umoja wa Mataifa na Baraza la Usalama la umoja huo hazijachukua hatua yoyote ya maana ya kuzuia mauaji hayo ya kimbari ya Waislamu wa Myanmar.