SANAA,YEMEN

MUUNGANO  wa kijeshi unaoongozwa na Saudi Arabia umefanya mashambulizi ya angani nchini Yemen na kuwaua watu kumi wakiwemo watoto sita.

Wanaharakati walisema hayo na kueleza kuwa mashambulizi hayo yalifanywa kaskazini mwa mkoa wa Jawf ambao ni ngome ya waasi wa Kihouthi.

Wizara ya Afya inayosimamiwa na Wahouthi ilisema mashambulizi hayo ya angani yalilenga kijiji cha Masafa ambacho waasi walichukua udhibiti wake mnamo mwezi Machi kutoka kwa vikosi vya serikali ya Yemen inayotambuliwa kimataifa.

Hakukuwa na tamko la moja kwa moja kutoka kwa muungano huo unaoongozwa na Saudi Arabia na ambao ulikuwa ukikosolewa kimataifa kuhusiana na mashambulizi yake ya angani dhidi ya shule, hospitali, sherehe za harusi na kusababisha vifo vya maelfu ya raia.