NA NIZAR VISRAM
MAANDAMANO yamekuwa yakiendelea nchini Marekani. Yalianza baada ya kuuawa kwa Mmarekani mweye asili ya Afrika, George Floyd mnamo Mei 25 mwaka huu katika jiji la Minneapolis, jimboni Minnesota.
Polisi wa kizungu walimvamia Floyd, wakamuangusha chini na mmoja kati yao, Derek Chauvin akamkandamiza kwa kumuekea goti shingoni, huku polisi wenzake wawili wakimshikilia Floyd hadi kukata roho.
George Floyd alipiga mayowe mara 11 akisema anashindwa kupumua, lakini Chauvin aliendelea kumkandamiza kwa muda wa takriban dakika tisa hadi alipokata roho.
Floyd hakuwa na silaha wala hakuwashambulia mapolisi hao. Mauaji ya Floyd yalirikodiwa kwa kutumia simu ya mkononi na mara moja video hiyo ikasambazwa katika mtandao wa kijamii duniani kote.
Hasira zilipanda juu na maelfu ya wananchi walimiminika mitaani katika miji zaidi ya 75 nchini Marekani. Mikutano ya kuuaga mwili wa Floyd ilifanyika katika miji mitatu, pamoja na Minneapolis. Polisi watatu wakafikishwa mahakamani na wakafunguliwa mashtaka ya mauaji ya Floyd. Jaji akawaachia kwa dhamana na ndipo hasira zikazidi kupanda.
Maandamano makubwa yalifanyika katika miji kama New York, Boston, Seattle, Miami, New Orleans, Washington, St-Louis, Los Angeles, Atlanta, Cleveland, Minneapolis,Detroit, Lansing, Rockford, Syracuse, Philadelphia, Tampa, Milawaukee, Denver, Dallas, Little Rock, Houston, Phoenix, Salt Lake, na Chicago.
Wamarekani weusi wengi, wakiungwa mkono na weupe wapenda haki, walijitokeza wakilaani mauaji ya raia weusi yanayofanywa na polisi nchini mwao.
Polisi na wanajeshi wenye silaha nzito nao wakatumia mabomu ya machozi, pilipili, marungu na risasi. Walitumia hata helikopta na drone. Mamia ya waandamanaji walijeruhiwa na wakakimbizwa hospitali. Watano wakafa. Hata wanahabari na wapita njia hawakuachwa.
Katika miji 39 polisi wakatoa amri ya kutotoka nje. Huduma za mabasi zikasimamishwa katika majiji kama New York na Chicago. Maelfu ya waandamanaji walikamatwa na kutiwa gerezani.
Mjini Chicago peke yake walikamatwa zaidi ya watu 1,000, Los Angeles 500, New York 300 na Dalas 84. Hata hivyo polisi walishindwa kuzuia maandamano yaliyokuwa yakienea nchini kote.
Wakati mmoja maandamano ya amani yalipokaribia ikulu (Washington), rais Donald Trump alikimbia na akajificha katika handaki lilioko chini ya ikulu. Baadae Trump akaamrisha uchunguzi ufanywe ili kumkamata aliyevujisha siri hiyo kwa wanahabari.
Maandamano ya Marekani yakaenea duniani kote. Yalifanyika huko Ujerumani ambako maelfu ya wananchi waliandamana hadi ubalozi wa Marekani mjini Munich na Berlin. Walilaani siyo tu mauaji ya Floyd bali pia ufashisti unaoenea kimfumo nchini Ujerumani. Mfano mmoja ulitolewa wa Oury Jalloh aliyeuawa gerezani kwa kuchomwa moto.
Maelfu ya wananchi waliandamana pia nchini Denmark, Italia, Israel, Uingereza na Canada. Nchini Palestina wananchi walilaani siyo tu mauaji ya Lyod huko Marekani bali pia ya Iyad Halak, Mpalestina mlemavu aliyeuliwa kwa risasi na wanajeshi wa Israel mjini Jerusalem (Al Quds).
Nchini Uingereza maandamano makubwa yalifanyika jijini London, Manchester na Birmingham. Waingereza walilaani mauaji yanayofanywa na polisi nchini mwao. Walisema mnamo 2017-2018 raia 283 walipoteza maisha yao wakiwa mikononi mwa polisi.
Jijini London, katika muda wa miezi mitano mnamo 2018, kulikuwa na matukio 41,477 ya polisi wakitumia nguvu kuwashambulia raia. Walitumia silaha inayotumia umeme (taser) mara 2,663 na risasi za moto mara 591. Ni wastani wa matukio manne kila siku.
Nchini Japan wananchi waliunga mkono maandamano ya Marekani na wakalaani pia polisi wa Tokyo kumuua mfanyakazi kutoka Kurdistan, mwenye umri wa miaka 33. Video ilionesha jinsi kijana huyo asiye na silaha akigandamizwa chini na polisi wawili.
Na katika miji ya Sydney, Melbourne na Brisbane, nchini Australia, maelfu ya waandamanaji walilaani mauaji yanayofanywa na polisi nchini mwao dhidi ya wazawa wenye asili ya nchi hiyo (Aborigine). Nchini New Zealand maandamano yalifanywa katika miji ya Auckland, Wellington, Christchurch na Dunedin.
Umoja wa Afrika (AU) ukatoa tamko rasmi tarehe 29 Mei kutoka makao yake makuu jijini Addis Ababa. Mwenyekiti wa tume ya umoja huo, Moussa Faki Mahamat, alilaani mauaji ya Floyd, akisema AU inatoa rambirambi kwa familia yake.
Alikumbusha azimio la Umoja wa Nchi Huru za Afrika (OAU) likilaani ubaguzi wa rangi nchini Marekani. Azimio hilo lilipitishwa na marais wa Afrika katika mkutano wao wa kwanza jijini Cairo tarehe 17 hadi 24 Julai 1964.
Mahamat alisema tangu wakati huo Afrika imekuwa ikilaani ubaguzi unaoendelea nchini Marekani dhidi ya raia weusi. Akautaka utawala wa nchi hiyo kuendelea na “jitihada zake” za kuutokomeza ubaguzi wa rangi.
Nchini Afrika Kusini maandamano yalifanyika nje ya bunge mjini Cape Town ili kulaani sera ya ukaburu dhidi ya weusi wa Marekani. Na mjini Johannesburg chama cha EFP kinachoongozwa na Julius Malema kilitoa tamko likilaani “mauaji ya kikatili ya George Floyd yaliyofanywa na polisi wa kikaburu nchini Marekani”.
Chama ch EFP kilisema mauaji haya ya Floyd ni matokeo ya ubaguzi mkubwa unaoambatana na utumiaji wa nguvu dhidi ya raia weusi unaoendeshwa na vyombo vya dola nchini Marekani.
Chama kikamtaka Rais Ramaphosa wa Afrika Kusini amuite balozi wa Marekani nchini Afrika Kusini na kumtaka serikali yake iache kutumia nguvu za kijeshi dhidi ya waandamanaji nchini Marekani.
Mauaji ya Floyd yalilaaniwa pia na wananchi wa Congo, Nigeria, Zimbabwe, Kenya na Uganda. Waafrika wamekumbusha jinsi raia wa Guinea, Amadou Diallo, alivyopigwa risasi 41 na polisi jijini New York mnamo 1999.
Mkuu wa tume ya haki za binadamu katika Umoja wa Mataifa, Michelle Bachelet ametoa ripoti yake kuhusu kuuawa kwa Floyd. Ripoti hiyo inasema:
“Mauaji ya Floyd ni moja tu kati ya orodha ndefu ya Wamarekani weusi wasio na silaha wanaouliwa na polisi nchini Marekani. Nasikitika kuwataja watu kama Breonna Taylor, Eric Garner, Michael Brown, Ahmaud Arbery, Trayvon Martin na wengine wengi ambao wamekufa wakiwa mikononi mwa polisi”.
Ni kweli kama asemavyo Bachelet kuna wengine wengi. Kwa uchache tunaweza kuongeza majina ya Sandra Bland, Tamir Rice, Yvette Smith, Laquan McDonald, Tanisha Anderson, Akai Gurley, Jerame Reid na Natasha McKenna.
Wengine ni Eric Harris, Walter Scott, Freddie Gray, William Chapman, Sandra Bland, Darrius Stewart, Samuel DuBose, Janet Wilson, Calin Roquemore, Alton Sterling, Philando Castile, Joseph Mann, Terence Crutcher, Chad Robertson, Jordan Edwards, Aaron Bailey, Stephon Clark, Danny Ray Thomas, Antwon Rose, Botham Jean, Atatiana Jefferson na Michael Dean.
Ahmed Aubrey, kwa mfano alikuwa akifanya mazoezi ya kukimbia (jogging) katika maeneo anakoishi. Polisi walipomuona wakamchukulia kuwa ni mwizi anayekimbia na wakampiga risasi na kumuua. Ni dhahiri kuwa mawazo potofu ya polisi yalitokana na Aubrey kuwa raia mweusi.
Ukweli ni kuwa kila mwaka nchini Marekani zaidi ya raia 1,000 wanauliwa na polisi. Idadi ya raia weusi kati yao ni mara tatu zaidi kuliko weupe. Pia weusi wengi wao wanauliwa wakiwa hawana silaha, tofauti na weupe. Cha kusikitisha ni kuwa asilimia 99 ya polisi wanaowauwa raia hawashitakiwi wala kufikishwa mahakamani.
Mauaji ya Floyd, kwa hivyo, hayakuwa ya kwanza nchini Marekani. Nchini humo limekuwa jambo la kawaida kwa polisi kutumia nguvu za ziada na silaha dhidi ya weusi.
Kwa mfano, mwaka 2014 askari polisi jijini New York alimuangusha chini Eric Garner. Akambamiza uso wake huku Garner akipiga mayowe mara 11, akisema anashindwa kupumua (kama alivyofanya Floyd).
Kosa lake eti alikuwa akiuza sigara mitaani bila ya kulipa kodi. Pia Lino Rivera, mwenye umri wa miaka 16, alikamatwa kwa kosa la kuiba kisu chenye thamani ya senti 10 za Marekani. Naye akauawa.
Kufuatia maandamano kote nchini Marekani, Rais Dolad Trump alitoa amri kwa polisi kuwa wakali na kutumia nguvu. Alisema maandamano yamepangwa na kikundi cha “magaidi, wahuni na wavuta bangi”.
Trump alitishia kuwa angetumia wanajeshi ili kuwadhibiti “wahuni.” Polisi nao wakatiwa moyo na wito huo wa rais wao na ndipo wakazidi kuwashambulia waandamanaji wasio na silaha.
0658- 010308