NA TATU MAKAME

JESHI la polisi mkoa wa Kaskazini Unguja, linamshikilia Omar Hamad Haji (30) mkaazi wa Chaani Bandamaji Wilaya ya Kaskazini ‘B’ Unguja kwa tuhuma za kupatikana na kete 60 za dawa za kulevya aina ya heroin.

Kaimu Kamanda wa polisi mkoa huo, Mussa Ali Mussa alisema tukio hilo lilitokea Julai 19 mwaka huu majira ya saa 11:30 jioni Kiwengwa Mafarasi.

Alisema mtuhumiwa huyo alipatikana na dawa hizo zenye uzito wa gramu 1.32 akiwa amezifunga kwenye kifuko cha plastiki na kuzihifadhi ndani ya suruali yake aliyokuwa ameivaa.

Alieleza kuwa mtuhumiwa huyo alikamatwa kufuatia operesheni iliyofanywa na jeshi hilo mkoani humo ikiwa ni sehemu ya kupambana na wasambazaji, wauzaji na watumiaji wa dawa za kulevya.

“Pamoja na mafanikio tuliyoyapata, Kikosi hicho kitaendelea na operesheni ili kuwadhibiti watu wanaoendeleza biashara hii ndani ya mkoa huu,” alieleza kamanda Mussa.

Aidha Kaimu Kamanda Mussa aliwataka masheha kushirikiana na jeshi la polisi katika mapambano ya dawa za kulevya na wananchi watoe taarifa pale wanapowabaini vijana wanajihusisha na biashara hizo.

Hata hivyo aliwataka vijana kuacha kujihusisha na utumiaji na usambazaji wa dawa za kulevya badala yake watafute kazi nyengine za kufanya kwani jeshi lake halitawafumbia macho.