KIJA ELIAS, HAI

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Hai  Mkoani Kilimanjaro,  kimemtaka Mbunge aliyemaliza muda wake na Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Freeman Mbowe, kujiandaa kutafuta kazi nyingine baada ya Oktoba 28 kutokana na kushindwa kulitendea haki jimbo hilo kwa miaka yote aliyokuwa mbunge.

Kauli hiyo ilitolewa jana na Mwenyekiti wa CCM wilayani humo Mang’uba Wanganda, wakati akizungumza katika mkutano wa kura za maoni kwa watia nia katika nafasi za Ubunge kwa tiketi ya chama hicho katika jimbo la Hai mjini ambao walifikia 41.

Wanganda alisema Jimbo la Hai limekuwa mikononi mwa upinzani kwa miaka kumi huku wakazi wake hali zao wakisalia kwenye giza nene hususani katika maendeleo yao ambayo waliahidiwa kutekelezewa na Mbunge huyo atakapokuwa madarakani.

“Wana CCM, tunasema kuwa tumechoka kukaa gizani kwa miaka kumi imepita tumekuwa na Mbunge Freeman Mbowe kutoka upinzani, lakini hatujaona maendeleo yeyote aliyoyaleta jimboni humu, giza nene limezi kutanda kwa wakazi wa wialaya ya Hai,”alisema.