NA MWANDISHI WETU,
KAIMU Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Ranchi ya Taifa (NARCO), Masele Mipawa amemsimamisha kazi Meneja wa Ranchi ya West Kilimanjaro iliyopo Arusha, Hezron Kyaruzi kwa tuhuma za kukosa uadilifu kwa mali za Umma na kusababisha upotevu wa Ng’ombe takriban 32.
Akiwa katika ziara ya kutembelea Ranchi hiyo ya West Kilimanjaro mwishoni mwa wiki, Mipawa alisema kuwa waliamua kufanya maamuzi hayo kufuatia changamoto nyingi zinazoikumba shamba hilo ambazo kwa kiasi kikubwa zimechangiwa na uongozi mbovu wa Meneja huyo.
“Kutokana na upotevu wa Ng’ombe, uzembe na ukosefu wa maadili tumeamua kumsimamisha kazi Meneja wa Ranchi na Msaidizi wake na hatua nyingine za kisheria na kinidhamu zitafuata,”alisema Mipawa
Mipawa alisema ziara hiyo aliyoifanya katika Ranchi hiyo ni kufanya ukaguzi kutokana na taarifa walizokuwa wakizipata ambazo zilionesha kuwa katika shamba hilo kumetokea upotevu wa Ng’ombe ambao Kampuni ya NARCO haina taarifa nao.
“Ziara hii imetusaidia kubaini kuwa kuna wizi uliokithiri katika shamba hili ambao umechangiwa na mahusiano mabovu kati ya Meneja na jamii inayozunguka shamba hili, ukosefu wa maadili na uadilifu wa Meneja ambao umepelekea Ng’ombe 32 kupotea,”alisema