BARCELONA, Hispania
KOCHA, Quique Setien amelazimika kukaa kitako na nahodha wake, Lionel Messi kumaliza tofauti zao na kupanga jambo moja tu, kuipa klabu taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu huu.

Miamba hiyo ya Nou Camp imekuwa kwenye kiwango cha chini tangu ligi iliporejea, ambapo wamepoteza ubingwa mbele ya Real Madrid.

Messi amekuwa akikosoa mbinu za Setien pamoja na wachezaji wenzake, kwamba wamekuwa dhaifu, hasa baada ya kipigo kutoka kwa Osasuna ambacho kiliwatibulia kwenye mbio za ubingwa.

Lakini, mchezo wao wa mwisho kwenye La Liga, walimaliza kwa hasira, waliposhinda 5-0 dhidi ya Alaves.
Kwa mujibu wa Mundo Deportivo, nguvu ya ushindi huo wa Alaves umekuja baada ya kufanyika kikao baina ya watu wawili hao wenye nguvu na waliokuwa na tofauti kubwa kwenye kikosi.

Bosi huyo wa Nou Camp alikutana ana kwa ana na Messi na kufanya mazungumzo na kumaliza ofauti zao na kuibuka na msimamo mmoja wa kuhakikisha Barcelona inabeba taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu huu.(AFP).