Mgombea urais wa Z’bar kwa tiketi ya CCM 2020

Ni mwanasiasa aliyekomaa, mbobevu kitaaluma

NA MWANDISHI WETU

MARA baada ya Chama cha Mapinduzi (CCM), kuwatangazia makada wake wenye nia ya kugombea urais wa Zanzibar, watu kadhaa walijitokeza kujaribu kuipata fursa hiyo.

Kuanzia Juni 15 mwaka 2020 makada wa CCM walianza kupisha mmoja baada ya mwengine na kufikia jumla ya wanachama 32 waliokwenda katika ofisi ya Kisiwandui kujitokeza katika ofisi ya organizesheni kuchukua fomu.

Kwenye mchakato wa uchukuaji fomu yapo majina yaliyokuwa yakitajwa kwa muda mrefu kwamba yangejitokeza, kwa bahati nzuri baadhi ya majina hayo yalijitokeza kuchukua fomu za kuomba nafasi hiyo.

Kwa upande wa pili pia walijitokeza makada wa CCM ambao sio tu  hawakutarajiwa kwenda kuchukua fomu, lakini pia hawakufikiriwa kama wangejitokeza kuchukua fomu za kuwania urais wa Zanzibar.

Katika moja ya jina ambalo kwa muda mrefu lilikuwemo kwenye orodha  kwamba litajitokeza katika mchakato wa kuwania urais wa Zanzibar mwaka 2020, lilikuwa na Dk. Hussein Ali Hassan Mwinyi.

Wakati wa kuchukua fomu kuomba ridhaa ulipowadia Dk. Hussein Mwinyi akawa miongoni mwao na mara baada ya kuchukua fomu na kutoka nje ya ofisi alikutana na waandishi wa habari ambao walikuwa na kiu ya kujua mengi kutoka kwao.

Hakuwapuuza waandishi hao wa habari, bali aliwaeleza kwa lugha ya upole sana “ nakuombeni sana leo niachilieni nikazisome hizi fomu nizifahamu halafu tutatafuta siku tutaelezena kwa kirefu”,alisema.

Mchakato wa uteuzi na mchujo uliendelea, kamati maalum ya halmashauri kuu ya CCM Zanzibar ilikutana Julai 4 ambapo pamoja na mambo mengine ilichuja walioomba fomu kutoka watu 31 (mmoja alijitoa) na kupata watano bora.

Watano bora wakafikishwa mjini Dodoma katika kikao cha kamati kuu ya halmashauri kuu ya taifa ya CCM mnamo Julai 9 ambayo ilipuunguza kutoka watano hadi kuopata watatu bora na majina yao kupelekwa katika kikao cha halmashauri kuu ambayo ilikuwa na kazi ya kumpata mtu mmoja.

Kamati kuu iliwasilisha majina matatu, Dk. Hussein Mwinyi, Dk. Khalid Mohammed Salum na Shamsi Vuai Nahodha na hivyo kuingizwa kwenye mchakato wa uwazi wa kupigiwa kura.

Matokeo yakamuwezesha Dk. Hussein kupata kura 129, Dk. Khalid kupata kura 19 na Shamsi Vuai Nahodha kupata kura 16 na hivyo, kwa matokeo hayo mnamo Julai 10 2020 chama kikampa ridhaa Dk. Hussein Mwinyi kuwa mgombea wa urais wa Zanzibar.

Bila shaka watu wanatamani kumjua Dk. Hussein Ali Mwinyi ni nani, hivyo katika makala haya japo kwa ufupi sana tumuangalie imekuja hadi kufika hapa alipo?

Dk. Hussein Ali Mwinyi, huyu ni mwanasiasa anayetoka katika familia ya rais wa Zanzibar awamu ya tatu kwa Zanzibar na awamu ya pili kwa Tanzania, mzee Ali Hassan Mwinyi ambaye nchini Tanzania anajulikana kwa jina la utani kama ‘mzee ruksa’.

Kwa sasa ni waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa katika serikali ya awamu ya tano, ameteuliwa katika baraza la mwanzo la mawaziri la Dk. John Magufuli, ambapo pia ni mbunge wa jimbo la Kwahani.

Kumbukumbu zinaonesha kuwa alizaliwa mnamo Disemba 23 mwaka 1966 Zanzibar ni mtoto wa mzee Ali Hassan Mwinyi na mama Sitti Mwinyi ambaye aliwahi kuwa ‘first lady’ katika awamu ya pili.

Dk. Mwinyi alianza elimu ya msingi jijini Dar es Salaam kati ya mwaka 1972 – 1976 akisoma katika skuli ya msingi Oysterbay jijini Dar es Salaam na mnamo mwaka 1984 hadi 1985 wazazi wake walimhamishia Misri ambako aliendelea na masomo ya elimu ya msingi hadi kuhitimu katika shule ya msingi “Manor House Junior”.

Skuli hiyo ilikuwa na hadhi ya “Middle School za Tanzania” kwa wakati huo. Hussein Mwinyi alipelekwa Misri kwa sababu baba yake (Ali Hassan Mwinyi) alihamishiwa nchini Misri kikazi kama balozi wa Tanzania nchini humo kwa  wakati huo.

Hussein Mwinyi alirejea Tanzania na kuendelea na masomo ya sekondari katika skuli ya sekondari Azania ambako alisoma kidato cha kwanza hadi cha nne mwaka 1982 – 1984.

Alipohitimu kidato cha nne alifaulu na kujiunga na skuli ya sekondari Tambaza kusoma kidato cha tano na cha sita, hata hivyo aliishia kusoma kidato cha tano peke yake mwaka 1984/1985, mwaka huo huo 1985 alikwenda nchini Uturuki kusomea utabibu wa binadamu.

Alianza masomo ya udaktari nchini Uturuki mwaka 1985 katika chuo kikuu cha utabibu cha Marmara na kuhitimu shahada ya utabibu wa binadamu mnamo mwaka 1992.

Kwa sababu hakumaliza kidato cha sita, alipokuwa nchini Uturuki alilazimika  kufanya masomo ya mwaka mmoja ya kujiandaa na udahili wa chuo kikuu “Pre University Studies”.

Mwaka 1993, Mwinyi alikwenda nchini Uingereza kujiendeleza zaidi kielimu, aliendelea na masomo ya juu ya utabibu katika Hospitali ya Hammersmith ambako alihitimu shahada ya uzamili ya utabibu mwaka 1994 na kuunganisha shahada ya uzamivu ya udaktari hapohapo Hammersmith ambayo aliihitimu mwaka 1997.

Dk. Mwinyi hakuishia tu kuwa daktari wa vyeti vya masomo bali aliitumikia fani hiyo kwa kufanyakazi za udakari na kusaidia jamii kuepukana na maradhi mbalimbali yaliyokuwa yakiwasumbua.

Alipohitimu shahada ya kwanza ya utabibu alirejea Tanzania na kufanya kazi kwa mwaka mmoja katika hospitali ya Taifa Muhimbili iliyopo jijini Dar es Salaam.

Na hata baada ya kuhitimu shahada ya uzamivu nchini Uingereza, alirejea nchini kwa mara nyingine na kufanya kazi katika hospitali ya chuo Kikuu cha Kumbukumbu ya Herbert Kairuki (HKMU) kwa miaka miwili.

Alijitosa rasmi kwenye siasa mwaka 1999 akiliwania jimbo la Mkuranga mkoani Pwani na kushinda, alipokuwa mbunge, Rais Benjamin Mkapa alimteua kuwa Naibu Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, alikaa katika wadhifa huo hadi mwaka 2005.

Kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka 2005, Dk. Mwinyi alijitosa tena jimboni, lakini safari hii siyo Mkuranga. Ilikuwa ni jimbo la Kwahani, Zanzibar – ambako alipambana na kuwashinda wagombea sita kutoka vyama vingine akipata kura 6,239 sawa na asilimia 85.6 akifuatiwa na Mussa Haji Khamis wa CUF aliyeambulia kura 921 sawa na asilimia 12.6.

Baada ya kuwa mbunge kwa mara ya pili, serikali ya awamu ya nne chini ya uongozi wa Jakaya Kikwete na Dk. Mwinyi ilimteua kuwa waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais na alidumu hadi mwaka 2008 alipohamishiwa wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa alikokaa hadi mwaka 2010.

Mwinyi alirejea tena na kugombea ubunge katika jimbo la Kwahani mwaka 2010, akashindana na hasimu wake wa mwaka 2005, Haji wa CUF, mara hii vyama vingine havikuweka wagombea akashinda kwa kura 5,277 sawa na asilimia 83.0 dhidi ya kura 1,085 sawa na asilimia 17.0 za CUF.

Mara baada ya uchaguzi wa mwaka 2010 Rais Kikwete akamteua Mwinyi kuwa Waziri wa Ulinzi kabla ya kumrejesha Wizara ya Afya mwaka 2012 na miezi 19 baadaye (yaani Januari, 2014) kwa mara nyingine tena akamteua kuwa Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, nafasi aliyodumu hadi mwaka 2015.

Katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015, Dk. Mwinyi alirudi tena katika jimbo la Kwahani, ikiwa ni mara ya nne akisaka nafasi ya kuwawakilisha wananchi, akafanikiwa kumshinda Khalid Rajab Mgana wa CUF na kuchaguliwa kuwa mbunge kwa kipindi cha nne.

Rais John Pombe Magufuli akamteua Mwinyi kuwa Waziri wa Ulinzi na Kujenga Taifa na hivyo kumuongezea rekodi ya kuongoza wizara hiyo kwa muda mrefu.

Mnamo mwaka mwaka 2015, Dk. Mwinyi alitajwa sana kama mmoja wa wanasiasa wanaoweza kuvaa viatu vya JK ikiwa CCM ingeamua mrithi huyo atokee upande wa Zanzibar, hata hivyo yeye mwenyewe hakuwa na nia na hakuchukua hata fomu.

Ndani ya CCM, Dk. Mwinyi anashikilia nyadhifa mbalimbali, mwaka 2000 aligombea na kushinda ujumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM (NEC), akashinda tena mwaka 2007 na kushinda na tangu wakati huo aliteuliwa kuingia kwenye kamati kuu ya CCM.

Dk. Mwinyi ni mmoja kati ya mawaziri wenye rekodi za kuwa shahada tatu za ubobezi wa taaluma na elimu ya juu katika fani moja. Amesoma kwa uhakika na ni mtu mwenye uwezo wa kutumia stadi za ubobezi wake kujenga weledi wa jumla.

Ni mmoja kati ya watu wapole, lakini wachambuzi wengi wa masuala ya siasa wanamuelezea kuwa upole wake hautakuwa kikwazo katika kuiongoza Zanzibar na kushindwa kuchukua hatua hasa kwenye masuala magumu yenye kuhitaji maamuzi magumu.

Aidha upole wake unaelezwa kuwa umeficha busara na hekima alizonazo sifa ambazo kwa hakika lazima kiongozi anayeongoza watu awenazo na kwamba upole wake si udhafu kama wengi wanavyodhani na kufikiria.

Wakati anawashukuru wajumbe wa halmashauri kuu ya CCM katika ukumbi wa makao makuu ya CCM ‘White House’, alitoa ahadi nzito moja ni kuhakikisha analinda mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964.

Hili ndilo jambo adhimu kwa wazanzibari ambao wanaamini mapinduzi hayo yaliyosimamisha nchi yao yaliyowapa uhuru wao yana kila sababu ya kulindwa kutunzwa na kuenziwa.

Dk. Mwingi alielezea dhamira yake ya kudumisha muungano, hii ni ahadi nyengine ambayo inatufanya tuendelee kuitwa watanzania popote tuendapo hapa ulimwenguni.

Muungano wa Tanzania ni kitu kisichoweza kufutika umetoka kuwa muungano wakisiasa sasa umekuwa muungano wa kiuchumi na kijamii watu wamezidisha mashirikiano kutokana na muungano.

Ahadi nyengine aliyoitoa katika mkutano huo suala zima la kuhakikisha anakwenda kuitekeleza na kuisimamia ilani ya uchaguzi ya mwaka 2020-2025, hili ni jambo muhimu kwa sababu CCM ndicho chama pekee chenye kuweza kuwaletea maendeleo visiwani Zanzibar.

Pamoja na hayo tunaelewa ana mipango mingi kwa Zanzibar na mengine mengi anaweza kuyatekeleza hasa ikizingatiwa kuwa anaelewa shida, dhiki, changamoto, raha za wazanzibari.