NA MWANDISHI WETU

UTAFITI wa maendeleo ya uwezeshaji kupitia mfumo wa benki za kiislamu (Islamic Finance Development report) ya mwaka 2017 inaonesha sekta ya uwezeshaji kwa mfumo wa kiislamu duniani inatarajiwa kuendelea kukuwa kwa kasi.

Ripoti ya utafiti huo, imebainisha kuwa hadi kufikia mwaka 2022 mfumo huo unaweza kukuwa hadi kufikia dola za kimarekani Trilioni 3.8 kutoka dola Trilioni 2.2 iliyorekodiwa mwaka 2016.

Hivyo matarajio ya ukuaji huo yanaonesha mfumo wa benki za kiislamu duniani ni wenye kukidhi kwa ufanisi mkubwa mahitaji ya kibiashara na shughuli za kiuchumi zinazofanywa na jamii.

Kwa hapa nchini benki ya Amana ni benki ya kwanza inayoendeshwa kwa kufuata mfumo wa fedha wa kiislamu unaozingatia misingi ya sharia (Fiqh al muamalat).

Aidha mfumo huo unajumuisha benki za kiislamu, bima za kiislamu (Takaful) na masoko ya dhamana (Sukuk) katika uendeshaji wake.

Mpaka sasa benki hiyo ina matawi manane nchi nzima ambapo hivi karibuni Waziri wa fedha Dkt. Philip Mpango alizindua tawi jipya la benki hiyo katika mkoa wa Tanga.

Waziri huyo, anasema kuwepo kwa benki hiyo kunatoa fursa ya wananchi ambao walikuwa wanashindwa kutumia benki za kawaida kuanza kutumia benki ya Amana kwa ajili ya kuhifadhi fedha zao.

Anasema kutokuwepo kwa riba katika huduma zake za kifedha ni kichocheo kikubwa cha kukuza uwekezaji pamoja na uchumi wa wananchi hususani wale wa hali ya nchi.

Hivyo aliwataka watanzania kutumia fursa hiyo kwa huduma zinazotolewa na benki hiyo kwa ajili ya kujiendeleza kiuchumi na kuondokana na lindi la umaskini.

Anasema kuwa wakati huu ambapo serikali inatekeleza sera ya viwanda ni jukumu la benki hiyo kuhakikisha inasogeza huduma zake katika maeneo yote nchi ili wananchi na wawekezaji waweze kunufaika.

“Pelekeni huduma hadi katika maeneo ya vijijini huko ndipo ambapo kuna wananchi wengi ambao wanahitaji huduma hizo lakini wanakosa kutoka na umbali wa kuweza kufikiwa na benki”, aliwaasa Waziri Mpango.

Aidha waziri huyo aklionyeshwa kufurahishwa na namna ambavyo benki hiyo inatoa huduma ya mikopo yenye dhamana ya vikundi na kuwa mkombozi mkubwa kwa wananchi wa hali ya chini.

“Naamini uwezeshaji huo wa vikundi utaweza kuwa chachu ya maendeleo kwa wafanyabiashara wadogo hususani wajasirimali ambapo maeneo mengine wanakosa vigezo vya kukopesheka”alisema Dkt Mpango.

Hata hivyo Waziri wa fedha anasema kuwa licha ya mafanikio makubwa yaliyoko kwa sasa katika sekta ya mabenki na taasisi za fedha nchi zinakabiliwa na changamoto ya uwepo wa riba kuwa.

Anasema kuwa hali inasababisha wakati mwingine taasisi hizo kushindwa kujiendesha kwa ufanisi kutokana na kuelemewa na madeni ambapo wananchi wameshindwa kuyalipa kwa wakati.

“Ushahidi ni namna ambavyo tumeweza kufutia leseni mabenki saba kutokana kushindwa kujiendesha kwa ufanisi na hii inatokana na wakopaji wengi kukopa pasipo na malengo yaliyokusudiwa na kusababisha benki kubaki na mzigo wa madeni”, alisema Dkt Mpango.

Waziri huyo anaongeza kuwa ni vyema watanzania wakawa na tabia ya kukopa fedha kwa ajili ya malengo mahususi ya kujiendeleza katika shughuli za kiuchumi na sio kukosa malengo.

Huku akiwaasa watumishi wa taasisi za fedha kuhakikisha wanatoa mikopo kwa kuhakikisha wateja wao wamekidhi vigezo na masharti ili kuepuka kuwaingiza kwenye matatizo hapo baadae.

Vile vile Waziri Mpango alitumia fursa hiyo kuwaasa watumishi wa benki kuhakikisha wanafanyakazi kwa uadilifu na kuepuka kujingiza kwenye vitendo vya kiuhalifu.

Nae Mkurungenzi Mtendaji wa benki hiyo Dkt. Muslim Masoud anasema kuwa toka kuanzishwa kwake benki hiyo mwaka 2011 imefanikiwa kuongeza idadi ya wateja hadi kufikia 75,236.

Huku jumla ya amana zimeweza kufikia zaidi ya shilingi Bilioni 192, ambapo uwezeshaji kwa wateja mbalimbali imeweza kukuwa kwa kasi hadi kufikia kiasi shilingi Bilioni 143 mpaka kufikia mwezi Juni mwaka 2018.

Aidha Dkt Masoud alisema kuwa mpango mkakati walionano ni kuhakikisha wanawafikia wateja wengi zaidi na kuwajumuisha katika huduma za kifedha hususani wanachi wa kipato cha chini.

“Tumewawezesha mikopo wafanyabiasha wadogo kupitia (Micro Finance) kuanzia mwezi Julai 2016 hadi mwezi Juni mwaka huu kiasi cha mikopo yenye thamani ya shilingi Biloni 6.2”, alisema Dkt Masoud.

Vile vile alisema kuwa benki hiyo haitoi mikopo ya fedha taslimu kama sehemu ya uwekezaji wake bali huwawezesha kiuchumi wateja wake kupitia shughuli au miradi wanaoifanya.

“Kutoa mikopo ya fedha taslim kwa njia ya riba hupelekea baadhi ya wakopaji kutumia fedha kinyume na malengo ya mikopo husika lakini kwa Amana benki huyo mikopo ambayo imethibitika kutokuwa na madhara kwa jamii”, alibainisha Mkurungenzi huyo.

Hata hivyo katika kuongeza kasi ya ujumuishi wa huduma ya kifedha kwa watanzania wa kipato cha kati na chini benki hiyo inatarajia kuanza uwezeshaji kwa vikundi vya wafanyabiashara wadogo.

Kwa upande wake Mkuu wa mkoa wa Tanga, Martine Shigela, alitumia fursa hiyo kuwaomba Benki hiyo kuhakikisha wanashiriki katika shughuli za huduma kwa jamii kama vile elimu na afya.

Anasema kuwa ili wananchi wa Tanga waweze kuona benki hiyo ni sehemu yao ni mihumi kuhakikisha wanasaidia miradi ya jamii kwa ukaribu.

“Tanga tunashughuli nyingi lakini ili wanatanga waweze kujua kama hii ni benki yao hamna budi kuanza kuchangia katika shughuli za kimendeleo kama vile ujenzi wa madarasa lakini na miundombinu ya vituo vya afya na zahanati”, alisema mkuu huyo wa mkoa.

Anasema kuwa uwepo wa benki hiyo utaweza kuchochea fursa ya viwanda mkoani huo lakini utaratibu wa kutoa vitendeakazi badala ya fedha nalo ni jambo zuri zaidi.

Mkuu wa mkoa huyo alisema kuwa utaratibu huo wa utoaji wa mikopo katika benki hiyo iwapo utaweza kutumiwa na wannachi wengi wa mkoa huo utaweza kuwainua kiuchumi na kuleta maendeleo makubwa.

“Niwaombe tu benki ya Amana hakikisheni mnafika katika fursa za miradi mikubwa kama ya bomba la mafuta pamoja na kuwafikia wanachi wengi ili huduma zenu zipanuke lakini wakaazi wa Tanga waweze kunufaika”, alisema Shigela.